2014-12-10 09:32:33

Mwarobaini wa kashfa ya Escrow unachemka!


Rais Jakaya Kikwete kutoa maamuzi ya Escrow katika wiki moja Apokea Ripoti, nyaraka na maazimio ya Bunge Aagiza Ripoti ya CAG iwekwe wazi hadharani, haya ni kati ya masuala tete tunayokutaka uyasome kwa umakini!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea Ripoti, nyaraka na ushauri wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow na atavifanyia maamuzi katika wiki moja ijayo. Rais Kikwete ambaye alianza kazi Jumatatu, Desemba 8, 2014 baada ya mapumziko ya kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita, amepokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Umma (PAC) na Maazimio ya Bunge kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow.

Kufuatia kupokea nyaraka hizo, Rais Kikwete ameelekeza kuwa Ripoti ya CAG iwekwe hadharani kwa ajili ya umma kuweza kuisoma na kujua nini hasa kimesemwa na kupendekezwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Rais Kikwete ameelekeza kuwa Ripoti hiyo itangazwe kwenye magazeti yanayosomwa na watu wengi na kwenye mitandao ya kijamii, ili Ripoti hiyo iweze kupatikana kwa Watanzania wengi.

Rais Kikwete ameanza kupitia na kusoma nyaraka hizo na katika wiki moja ijayo atazitolea maamuzi kwa maana ya kwamba yale mambo yanayomhusu yeye moja kwa moja atayatolea maamuzi yeye, yale yanayohusu Serikali atayatolea maagizo na maelekezo ya namna ya kuyashughulikia.

Wakati huo huo, Rais Kikwete Jumatatu, Desemba 8, 2014, alianza kazi rasmi baada ya afya yake kuimarika kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita. Mhe. Rais alianza kazi rasmi kwa kumwapisha Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Daudi Felix Ntibenda katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam. Kwa kuanzia Mhe. Rais atakuwa anafanya kazi za ofisini na kwa muda mchache. Muda na kasi ya kufanya kazi ya Mhe. Rais vitaongezeka kwa kadri afya yake inavyozidi kuimarika.

Na kwa sababu sasa ameanza kazi, Mhe. Rais ataanza kushughulikia mambo yale ambayo yamekuwa yanasubiri maamuzi yake. Rais Kikwete alifanyiwa upasuaji wa tezi dume katika Hospitali ya Johns Hopkins ya Baltimore, Maryland, Marekani Novemba 8, mwaka huu na alirejea nyumbani Novemba 29, mwaka huu. Tokea awasili nyumbani, Mhe. Rais amekuwa anafanya mazoezi asubuhi na jioni kuimarisha afya yake kama alivyoshauriwa na madaktari.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa Jumatatu, Desemba 8, 2014 amepokea ujumbe wa viongozi wa dini wa Mkoa wa Dar Es salaam, ukiongozwa kwa pamoja na Askofu Valentino Mokiwa wa Kanisa la Anglikana na Sheikh wa Mkoa wa DSM, Alhaj Alhad Mussa Salum. Viongozi hao walifika Ikulu, Dar Es Salaam kumjulia hali Rais Kikwete kufuatia upasuaji ambao alifanyiwa mwezi uliopita kwenye Hospitali ya Johns Hopkins, Baltimore, Maryland, Marekani.
Mbali na kumjulia hali, viongozi hao pia walimwombea dua na sala wakiomba Mwenyezi Mungu amjalie kasi ya kurejesha afya yake kamili na kuweza kuendelea na kazi ya kuwahudumia Watanzania. Rais Kikwete pia alitumia muda huo kuwaelezea viongozi hao kuhusu ugonjwa uliokuwa unamsibu na kusisitiza kuwa anakusudia kuchukua hatua zaidi za kuwahamasisha Watanzania kupima afya zao mapema ili kujua fika hali za afya zao.

“Mimi Mwenyezi Mungu aliniongoza kuweza kupima mapema na kugundua kuwa ilibidi nipatiwe matibabu ya haraka kuhusu saratani ya tezi dume (prostrate). Vinginevyo nisingejua. Nawashukuru kwa maombi yenu, nawashukuru kwa dua zenu. Daktari mkubwa ni Mungu na ndiye aliniongoza kufanya vipimo mapema,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kwa hakika, saratani inatibika lakini ni lazima igundulike mapema na inaweza kugundulika mapema kama tukifanya uchunguzi wa mara kwa mara wa afya zetu. Mimi nimenusurika kwa sababu nilipima mapema. Nataka tuanze kuwasaidia watu wengi zaidi wapime afya zao mapema.”








All the contents on this site are copyrighted ©.