2014-12-10 10:12:51

Mahojiano maalum na Rais Guebuza wa Msumbiji!


Mahusiano kati ya Vatican, Kanisa na Serikali ya Msumbiji katika mchakato wa maendeleo endelevu; haki, amani na upatanisho wa kitaifa; umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kudhibiti biashara ya silaha duniani ambayo imekuwa ni chanzo cha majanga makubwa kwa mataifa mengi; umaskini na ukosefu wa usawa kati ya watu; ni kati ya mambo msingi ambayo Rais Armando Emìlìo Guebuza wa Msumbiji pamoja na Baba Mtakatifu Francisko waligusia, walipokutana hivi karibuni mjini Vatican.

Rais Guebuza alikutana na kuzungumza na Radio Vatican anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwa namna ya pekee mchakato wa kuendeleza amani, utulivu na upatanisho wa kitaifa kama kikolezo cha maendeleo endelevu miongoni mwa wananchi wa Msumbiji ambao kwa miaka mingi wamejaribiwa na kuteseka kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Baba Mtakatifu anawachangamotisha wananchi wa Msumbiji kujifunga kibwebwe katika kupambana na umaskini wa hali na kipato, kwa kujiwekea mikakati ya maendeleo endelevu inayogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili; mambo ambayo hayana budi kujikita katika umoja na mshikamano wa kitaifa.

Rais Guebuza anasema, Msumbiji kama taifa changa ambalo limejaribiwa sana kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe bado halijawa na msingi thabiti wa umoja wa kitaifa, mwaliko kwa wananchi wa Msumbiji kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuheshimu tofauti zinazojitokeza kati yao na kwamba, tofauti hizi zisiwe ni kizingiti cha umoja wa kitaifa.

Serikali ya Msumbiji licha ya changamoto mbali mbali zilizopo, inaendelea kucharuka katika mikakati ya kuwaletea wananchi wake maendeleo endelevu kwa kutumia kikamilifu rasilimali iliyopo kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kujenga uchumu imara zaidi. Kwa miaka mingi, Italia imekuwa ni mwekezaji mkuu nchini Msumbiji na kwamba, imeonesha nia ya kuendelea kuwekeza zaidi na zaidi. Kwa sasa Shirika la Nishati la Italia, ENI linaendelea kufanya upembuzi yakinifu ili kuanza kuchimba gesiasilia ambayo inapatikana kwa wingi nchini Msumbiji.

Rais mpya wa Msumbiji Bwana Filipe Nyusi, anatarajiwa kuapishwa wakati wowote mwanzoni mwa mwezi Januari, 2015 baada ya kukamilisha mchakato wa kurithishana madaraka kadiri ya sheria na kanuni za nchi. Kwa sasa anasema Rais Guebuza yeye ndiye nahodha wa Serikali ya Msumbiji na kwamba, Rais mpya anatarajiwa kuendeleza mahusiano mema kati ya Msumbiji na nchi marafiki na kwamba, ni kiongozi ambaye anapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wake.

Bwana Nyusi ni kiongozi ambaye historia ya Msumbiji iko kiganjani mwake ni mtu ambaye anapenda kukuza na kudumisha mahusiano ya kirafiki na nchi jirani pamoja na zile zinazozungumza lugha ya Kireno.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.