2014-12-10 08:49:24

Chimbachimba na Baba Mtakatifu Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni alifanya mahojiano maalum na Gazeti la "La Nacion" linalochapishwa nchini Argentina, pamoja na mambo mengine muhimu, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kuhusu Familia; Mabadiliko katika Sekretarieti ya Vatican, Benki ya Vatican na maisha yake katika Hosteli ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican.

Katika mahojiano haya Baba Mtakatifu amemwambia Elizabetta Pique, mwandishi wa habari wa gazeti hilo kwamba, mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi hauna budi kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata wala kukatishwa tamaa, kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu anataka kuliambia nini Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Baba Mtakatifu anasema, Sinodi ni "jukwaa wazi ambalo linalindwa na kusimamiwa na Roho Mtakatifu" na kwamba, ulikuwa ni uzushi wa baadhi ya vyombo vya habari kwamba, Mababa wa Sinodi walikuwa wamegawanyika na kusigana wakati wa maadhimisho ya Sinodi. Mababa wa Sinodi walipata fursa ya kuzungumza wazi, katika ukweli, wakisikilizana na kuheshimiana katika unyenyekevu.

Familia inakabiliana na matatizo, changamoto na fursa nyingi ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi na Mama Kanisa, jambo ambalo linahitaji kufanyiwa upembuzi yakinifu. Kuna idadi kubwa ya waamini ambao walikuwa wameoa, wakaachana na kuolewa tena, hili ni kundi ambalo linahitaji kusaidiwa kikamilifu ili kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kama ambavyo aliwahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI. Hapa Kanisa linapaswa kuangalia uelewa wa waamini katika Sakramenti ya Ndoa; imani yao katika Sakramenti hii; haya ni mambo msingi katika udumifu wa Sakramenti ya Ndoa.

Kuhusu ndoa za watu wa jinsia moja, Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwamba, Mababa wa Sinodi hawakuzungumzia kuhusu ndoa za watu wa jinsia moja ndani ya Kanisa, kwani hiki ni kinyume cha Maandiko Matakatifu, Mapokeo na Kanuni maadili ya Kanisa. Mababa wa Sinodi wamezungumzia ni jinsi gani ambavyo Kanisa linaweza kuzisaidia familia zenye watoto wenye mielekeo ya ushoga au usagaji; tatizo ambalo linaendelea kukua na kukomaa kiasi hata cha kuonekana kana kwamba ni sehemu ya haki msingi za binadamu!

Mababa wa Sinodi wamezungumzia watu wenye maelekeo ya namna hii kadiri ya mahusiano yao ndani ya Familia, mambo ambayo Mapadre wengi wanakutana nayo katika Sakramenti ya Upatanisho. Haya yalikuwa ni mawazo yaliyotolewa na baadhi ya Mababa wa Sinodi katika hati yao elekezi, kumbe maamuzi ya Mababa wa Sinodi yamehainishwa barabara katika Hati yao ambayo kwa sasa imechapishwa kama hati elekezi na kutumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Duniani, tayari kwa maandalizi ya maadhimisho ya awamu ya pili ya Sinodi ya Maaskofu itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 25 Oktoba 2015.

Baba Mtakatifu anasema, mara baada ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kumekuwepo na: Ujumbe wa Mababa wa Sinodi kwa Familia ya Mungu, Hati ya Mababa wa Sinodi na Hotuba yake kwa Mababa wa Sinodi; mambo yote haya ni sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi, ambayo haina budi kusonga mbele bila kuogopa, kwani inaongozwa na Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, mwishoni amewaambia Mababa wa Sinodi kwamba, Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuhusu: Sakramenti ya Ndoa na maisha ya Kifamilia hakuna mabadiliko. Mababa wa Sinodi wametoa maoni mbali mbali kuhusu changamoto za wanandoa waliooa au kuolewa na baadaye wakaachika na kuamua kuoa au kuolewa tena, ili kuwasaidia waamini kushiriki vyema katika maisha na utume wa Kanisa.

Ni waamini ambao wanavikwazo kadhaa vinavyowanyima nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa; hawa Mama Kanisa hana budi kuwapatia tena nafasi walau waweze kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa. Ni kweli kwamba, baadhi ya waamini kama hawa si mfano bora wa kuigwa katika maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anasema, hapa hakuna kinzani wala kuchanganyikiwa, kwani mafundisho, maoni na msimamo wake katika maisha na utume wa Kanisa anaendelea kuyatoa katika: mahubiri ya kila siku, Waraka wa Injili ya Furaha pamoja na matamko mbali mbali kwa kusoma alama za nyakati.

Baba Mtakatifu anasema, mabadiliko kwenye Sekretarieti ya Vatican yanaendelea polepole kwani hili si jambo la mzaha linaloweza kukamilika ifikapo mwaka 2015. Baraza la Makardinali Washauri linaangalia jinsi ambavyo Sekretarieti ya Vatican inavyoweza kufanya kazi zake kwa ufanisi, weledi na taaluma kwa kuwa na idadi ndogo ya Mabaraza ya Kipapa, pale inapowezekana kuunganisha baadhi ya Mabaraza.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mabadiliko makubwa ambayo anapenda kuyapatia kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa ni toba na wongofu wa ndani; mabadiliko yanayogusa sakafu ya moyo wa binadamu. Kwa sasa anasema anaendelea kuandaa hotuba ya Noeli kwa ajili ya Sekretarieti ya Vatican na hotuba kwa wafanyakazi wote wa Vatican pamoja na familia zao, tukio litakalofanyika tarehe 22 Desemba 2014, kwenye Ukumbi wa Paulo VI.

Baba Mtakatifu anasema hakuna sababu ya kuogopa kuwa na maoni tofauti, kwani kwa sasa anachofanya ni kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Makardinali wakati wa Mikutano elekezi, iliyofanyika kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Benki ya Vatican kwa sasa inatekeleza vyema dhamana yake kwa kuzingatia ukweli, uwazi, weledi, uadilifu na uwajibikaji na kwamba, mageuzi katika mfumo wa uchumi nayo yanakwenda kadiri yaligvyopangwa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema katika umri wa miaka 77 si rahisi sana mtu kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yake, ndiyo maana ameamua kuendelea na maisha yake kama alivyokuwa kabla ya kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Umri wake pia unabeba pamoja na mambo mengine changamoto za kiafya, lakini yote anayaweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kwamba, anaendelea vyema na utaratibu wa kazi na utume wake kama kawaida. Kabla ya kuteuliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki alikwishaanza kujiandaa kwa ajili ya kung'atuka kutoka madarakani, ili kupata muda zaidi wa kuungamisha waamini waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anasema, panapo majaliwa, kunako mwaka 2016 anaweza kufanya hija ya kichungaji nchini Argentina, lakini kwa Mwaka 2015 kuna maandalizi yameanza kwa ajili ya hija ya kitume katika nchi za Amerika ya Kusini na Barani Afrika. Kufuatia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Argentina hivi karibuni, Baba Mtakatifu ameamua kutokutana na kuzungumza na wanasiasa kutoka Argentina, ili asiingilie mchakato wa uchaguzi, lakini anasema kwamba, kuvunjwa kwa mfumo wa demokrasia na ukiukwaji wa Katiba yanaweza kuwa ni "majanga" kwa wananchi wa Argentina.

Baba Mtakatifu Francisko anasikita kusema kwamba, kumekuwepo na upotoshaji wa makusudi kabisa kuhusu kusitishwa kwa huduma iliyokuwa inatolewa na Kamanda mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Vatican, kwamba amefukuzwa kazi! Habari hizi si za ukweli na ni uzushi wa hali ya juu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, anaheshimu huduma zilizotolewa na Kamanda wa Vikosi vya Ulinzi na usalama ambaye ameonesha uadilifu mkubwa, kuwa kweli ni mtu wa imani na baba mwema wa familia. Kamanda huyu alikuwa amekwishahitimisha muda wa huduma mjini Vatican na akaongezewa muda mwingine tena na kwamba, muda huu unakamilika Desemba 2014.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.