Waamini wa dini mbali mbali duniani wana wajibu wa kujenga na kudumisha amani!
Mkutano wa viongozi wa dini ya Kikristo na Kiislam uliowajumuisha wasomi na wanazuoni
kutoka sehemu mbali mbali za dunia, uliopania pamoja na mambo mengine kudumisha na
kuimarisha majadiliano ya kidini na kitamaduni, ili kuweza kukabiliana kikamilifu
na kinzani zinazojitokeza miongoni mwa waamini wa dini hizi mbili, umehitimishwa kwa
wajumbe kutoa tamko la pamoja linawataka waamini wa dini hizi kufahamiana zaidi, ili
kudumisha: haki, amani na utulivu.
Ujumbe wa Wakristo katika mkutano huu umeongozwa
na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini
na upande wa dini ya Kiislam, ujumbe wao uliongozwa na Mwana wa Mfalme El Hasan bin
Talal kutoka Yordan. Kauli mbiu iliyokuwa inaongoza mkutano huu ilikuwa “Wakristo
na Waislam waamini katika jamii”.
Waamini wa dini mbali mbali wanatambua changamoto
ya vita na kinzani za kidini inayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia,
hasa zaidi huko Mashariki ya kati, katika baadhi ya nchi za Kiafrika. Dini kwa sasa
inaonekana kuwa ni kichocheo cha vita na vurugu badala ya kuwa ni chombo cha haki,
amani na upatanisho kati ya watu. Wajumbe wameonesha furaha yao ya ndani kwa kukutana
na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, aliyewatia shime ya kuendelea kukutana
mara kwa mara ili kufahamiana na hatimaye, kujenga umoja na udugu.
Kabla ya
kuhitimisha mkutano huu, kulifanyika kikao cha hadhara ambacho kiliwashirikisha wanadiplomasia
kutoka katika nchi na Mashirika mbali mbali ya Kimataifa wanaoziwakilisha nchi zao
mjini Vatican bila kuwasahau waandishi wa habari, waliofahamishwa mkakati kazi utakaotekelezwa
na viongozi hawa kwa siku za usoni. Mkutano huu umeendeshwa katika mazingira ya kuheshimiana,
kwa kusikilizana, ili kukuza na kudumisha upatanisho, haki na udugu, mambo msingi
ambayo kwa sasa yanahitajika ulimwenguni.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.