2014-12-08 09:35:04

Pangua pangua ya Rais Kikwete!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Mkuu Mpya mmoja wa Mkoa na kuwahamisha vituo vya kazi wengine sita kuanzia Jumamosi, Desemba 6, 2014. Taarifa iliyotolewa Jumapili, Desemba 7, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue mjini Dar es Salaam inasema kuwa Rais amemteua Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha, Ndugu Daudi Felix Ntibenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Ndugu Ntibenda ameapishwa Jumatatu, Desemba 8, 2014, saa nne asubuhi, Ikulu, Dar Es Salaam. Taarifa hiyo inasema kuwa wakuu waliohamishwa vituo vya kazi ni Mheshimiwa Elaston Mbwilo anayehamishwa kutoka Mkoa wa Manyara kwenda Mkoa wa Simiyu ambako anachukua nafasi ya Mheshimiwa Paschal Mabiti aliyepewa likizo ya ugonjwa, Mheshimiwa Joel Nkanga Bendera aliyehamishiwa Mkoa wa Manyara kutoka Mkoa wa Morogoro na Mheshimiwa Dkt. Rajabu M. Rutengwe anayehamishiwa Mkoa wa Morogoro kutoka Mkoa wa Tanga.

Wengine ni Mheshimiwa Magalula Saidi Magalula anayehamishiwa Mkoa wa Tanga kutoka Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Mwantumu Bakari Mahiza anayehamishiwa Mkoa wa Lindi kutoka Mkoa wa Pwani na Mheshimiwa Mhandisi Evarist B. Ndikilo anayehamishiwa Mkoa wa Pwani kutoka Mkoa wa Arusha. Wakuu wengine wa mikoa wanaendelea kubakia katika vituo vyao vya sasa vya kazi.








All the contents on this site are copyrighted ©.