Kanisa liko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Ukimwi
Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, tangu mwaka 1989 limekuwa mstari wa mbele katika
mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi nchini Uganda, kwa kuhakikisha kwamba, Watu wa
Mungu wanapatiwa huduma makini, kwa kujali na kuzingatia heshima na utu wao kama binadamu.
Kwa kufanya hivi Kanisa linatambua sura ya Kristo mteswa kati ya wagonjwa, lakini
zaidi wagonjwa wa Ukimwi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda limekuwa likijitahidi
kukusanya takwimu za wagonjwa wa Ukimwi na wale wanaohudumiwa katika vituo vinavyosimamiwa
na kuendeshwa na Kanisa. Hadi sasa kuna zaidi ya wagonjwa 90, 646 wanaohudumiwa katika
vituo hivi, ingawa bado kuna vituo ambavyo havijaanza kutoa takwimu zake katika idara
ya takwimu za Kanisa Katoliki Uganda, unaojulikana kama DHIS2.
Makanisa mahalia
nchini Uganda kwa kutumia vituo vyake vya afya, yanaendelea kutoa huduma kwa Mama
na mwana, ili kudhibiti maambukizi ya virusi kutoka kwa Mama mjamzito kwenda kwa mtoto
wakati wa kujifungua na kampeni hii imesaidia kuokoa maisha ya watoto wengi ambao
kwa sasa wanazaliwa pasi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi. Lengo ni kuhakikisha
kwamba, walau Uganda inafanikiwa kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa
Mama kwenda kwa mtoto. Ili kuweza kufikia lengo hili kila mdau anapaswa kutekeleza
kikamilifu dhamana na wajibu wake mbele ya umma na familia katika ujumla wake.