2014-12-08 08:02:02

Ebo! Msiendekeze wala kufagilia kinzani na migawanyiko!


Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la Nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo! Leo tunalitazama agizo la Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican linalojulikana kwa jina la Orientalium ecclesiarum, agizo lililosheheni mitazama chanya na maelekezo mintarafu Makanisa Katoliki ya Mashariki.

Makanisa ya Kikatoliki ya Mashariki, ni jumla ya makanisa ishirini na mawili yenye kufuata riti ya pekee ya kiliturujia kadiri ya mapokeo ya tangu zamani za Historia ya dini Takatifu. Makanisa hayo yapo katika muungano kamili na Baba Mtakatifu, Askofu wa Roma, na hivyo pamoja na Kanisa la Roma, yanafanya sehemu ya Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki la Mitume.

Kwa sababu ya uhamaji na makazi, Makanisa hayo Katoliki ya Mashariki yamesambaa kutoka katika Ulaya Mashariki, Mashariki ya kati, Afrika ya Kaskazini na India, kuelekea Ulaya Magharibi, Amerika na kwingineko kote duniani. Hivyo, sio makanisa ambayo yamejifunga katika vigezo vya utaifa au Jiografia. Yana waamini popote na wote tunaongozwa na Baba Mtakatifu kama Khalifa wa Mtume Petro. Ni katika mtazamo huo, Mtaguso Mkuu, uliona ni vema kutoa mwongozo maalumu wa kimahusiano na makanisa hayo.

Kitaalimungu, Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, unayatazama Makanisa hayo Katoliki ya Mashariki kama Makanisa dada ya Kanisa la Roma. Yana hadhi sawa, na hivyo hakuna lililo na hadhi zaidi kuliko mengine, yana haki sawa na wajibu sawa na utume ni uleule wa kuhubiri Injili ya Kristo kwa kila kiumbe chini ya Uongozi wa Baba Mtakatifu. Katika kiti kitakatifu, Makanisa hayo yanawakilishwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, linayoongozwa na Kardinali Kiongozi, katibu wake pamoja na Makardinali 27, Askofu Mkuu mmoja na Maaskofu wanne.

Pamoja na kwamba Makanisa hayo yanatambua ukuu wa Askofu wa Roma kama Mrithi wa Mtume Petro na Kiongozi wa Kanisa zima Takatifu, bado wana haki ya kutunza mapokeo yao ya kiliturujia, sheria zao, desturi zao na mapokeo mbalimbali ya kiibada, na wana mikazo yao ya kipekee kiteolojia na kinidhamu.

Kwa kufuata taratibu maalumu, sisi wa Kanisa la Magharibi tunashirikiana na ndugu zetu wa Makanisa ya Mashariki. Mintarafu Sakramenti, Mtaguso Mkuu ulirudisha utaratibu wa kale wa kuweza kupokea baadhi ya Sakramenti kutoka kwa wahudumu wa riti za Makanisa Katoliki ya Mashariki, endapo wahudumu wa Kanisa lako hawapatikani katika mazingira hayo. Kwa mfano, endapo ukajikuta katika mazingira ya makanisa hayo, na Mapadre wa Kanisa lako hawapo, basi kwa ruhusa ya wakuu mahalia, unaweza kihalali ukapatiwa huko Sakramenti ya Ubatizo, kitubio na Kipaimara. Pia unaweza kushika kitakatifu siku ya Bwana na maisha yote ya kiibada kwa kushiriki Ibada katika Makanisa hayo.

Kwa ujumla wake Mtaguso Mkuu kwa njia ya hati hii, ulijaribu kufungua mlango mpana zaidi wa mahusiano kati ya Makanisa Katoliki ya Mashariki na Magharibi, na kujaribu kupunguza utengano wa tofauti ndogondogo zilizokuwepo. Mababa wa Mtaguso walihamasisha zaidi roho ya ushirikiano na roho ya sala ili kuendelea kuombea umoja ule aliouomba Kristo Bwana katika sala ile ya Kikuhani (Yoh. 17). Na mwisho kabisa hati inafungwa kwa kusisitiza juu ya upendo, heshima na kujaaliana zaidi kadiri ya mtazamo wa Kiinjili.

Lengo letu: Sauti hii ya mtaguso isikike katika Kanisa la Nyumbani. Cheche za mtaguso, zifike katika familia zetu. Tazama! Mababa wa Mtaguso hapa, wakiongozwa na hekima ya Kimungu, mintarafu Makanisa Katoliki ya Mashariki, kati ya mambo mengi walitazama yafuatayo: Kwanza kabisa, chanzo chetu ni kimoja. Sote tunatoka kwa Kristo yuleyule. Pili, utume wetu ni mmoja, yaani kuitangaza Injili ya Kristo kwa watu wote na tunayemtangaza ni Kristo yuleyule. Tatu lengo letu ni lilelile, yaani kupata wokovu wa milele. Kutokana hayo, mababa wa Mtaguso wanatufikirisha, iwapo tumeungana katika mambo ya msingi, kwa nini basi tusiheshimiane katika tofauti zetu zisizo za msingi?

Ndipo sasa, wanatoa mwongozo unaoweza kutusaidia sote kama Kanisa la Kristo tukaenda pamoja, huku tukitambuana na kujaaliana katika tofauti zetu za kihistroria na mapokeo ya kiibada, tukiheshimiana na kusaidiana ili tuufikie ule mwisho mwema. Wakayaangazia na kukayakazia zaidi mambo yanayojenga umoja, kuliko kukuza mambo yanayoendeleza chokochoko na utengano.

Na sisi katika familia zetu, kama wanavyokuwa wote wanaoanza maisha ya ndoa na familia, huanza kwa amani, furaha na umoja wenye simenti ya kutosha. Lakini polepole mambo yale ya msingi yanayoleta umoja huweza kubomolewa kwa uzembe au hila fulani za mwovu. Swali linakuja, je kuna juhudi makini ya kurudisha furaha na umoja uliokuwako pale mwanzo?’ Kuna jitihada za kuketi pamoja na kutafakari, ni wapi au ni nini kimetufanya tukawa na tofauti na namna gani tuziondoe tofauti hizi? Imani yetu ni kwamba, maisha mema ya furaha na amani yanawezekana kabisa. Na maisha hayo hayanunuliwi sokoni, bali yanajengwa na wanafamilia wenyewe, kwa kuketi, kujitathimini na kuchukua hatua.

Lakini pia lisisahauliwe suala la utofauti wa kijinsia, kihistoria, kitabia na mitazamo ya mambo. Ndiyo, kuna mambo ambayo ndani ya familia yanaweza kurekebishwa, lakini mengine inakuwa ni ngumu kabisa kuyarekebisha, tena sio kwa sababu ya kiburi bali kwa sababu fulani za kimsingi kabisa. Basi ikitokea hivyo, hapo ndipo upendo, uvumilivu na kuombeana kwa Mungu vishike nafasi.

Ukitaka tu mwenzako abadilike, awe kama wewe, afikiri kama wewe, atende kama wewe, hapo utakuwa unamkosea haki ya kuwa nafsi huru. Utakuwa unamkalia puani, atashindwa kupumua, hatakua na atakufa. Lakini katika kutambuana tofauti zetu na kusaidiana kuenenda kadiri ya tofauti zetu huku tukitunza yale mambo yaliyo ya msingi zaidi, hapo ndio Mungu hutukuzwa. Haiwezekani mwenzako akawa mtu mbaya tuu, hapana, ana jambo zuri, na wewe haiwezekani ukawa ni wa hovyo tuu, hapana una jambo jema. Hayo mema basi yakuzwe na yasaidie kujenga furaha yetu na umoja wetu. Tatizo ni kale katabia ka kukomalia vijitatizo vidogovidogo vya kila siku. Jambo dogo mwanandoa utalikuza na kuliimbaimba wee, hali linasikika kuwa ni kubwa.

Wakati mwingine tunagombana na kutengana katika familia kwa mambo madogo sana, na tunabaki na uhasama huo, tunajinyima raha na kujikaribishia magonjwa kwa muda mrefu kabisa. Kwa nini? Mwito kwa Kanisa la nyumbani linalodundadunda na kwa wote tulio katika mitafaruku, kujihoji: hivi tuna sababu halali ya kuwa na uhasama tulio nao? Tunalipwa chochote kwa kuendekeza chuki na vinyongo vya muda mrefu? Tutakuwa katika hali ya uhasama na migogoro mpaka lini? RealAudioMP3

Basi, tukifuata mfano huo wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliolenga kukuza umoja na ushirikiano zaidi ndani ya Kanisa, nasi basi katika familia zetu, tukuze umoja, upendo na mshikamano wetu.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.