Mpendwa mwanatafakari, tukiwa bado katika safari ya hija ya wokovu, maandalizi ya
roho zetu kumpokea Emanueli Mwana wa Mungu, Mama Kanisa haachi kutuwekea zawadi kichocheo
cha imani na furaha ya mioyo yetu. Zawadi hii ni fumbo la kukingiwa dhambi ya asili
Mama Bikira Maria, Mama wa Mungu.
Mpendwa,
wote twajua kabisa kuwa kwa njia ya Adamu tumeingia duniani, na katika hali ya kawaida
twajua kuwa roho ikiungana na mwili lazima ipate madhara ya mwili na hivi kwa jambo
hili dhambi ya asili. Je, inawezekanaje Mama huyu asipate dhambi hii? Swali hili limekuwa
likiulizwa tangu karne za kwanza za Kanisa mpaka hivi leo. Mama Kanisa akisali sana
na kujikabidhi mbele ya Mungu akitazama Neno la Mungu na mapokeo anaweka wazi ufunuo
wa Mungu mwenyewe akifundisha ulio ukweli wa ufunuo na kutangaza kuwa Bikira Maria
ni Mkingiwa dhambi ya asili.
Mama huyu anakingiwa dhambi ya asili kwa sababu
lazima awe makao stahili ya Mwana wa Mungu aliye mtakatifu, asiye na doa la dhambi.
Ndiyo kusema kwa vile Mwana wa Mungu ni mtakatifu asingeweza kuingia mahali pasipo
patakatifu. Kumbe kukingiwa dhambi ya asili kwa Mama Bikira Maria ni zawadi ya Kristo
mwenyewe kwa mama yake, na anaitoa zawadi hii mapema kwa mastahili ya msalaba atakaoupokea
baadaye.
Mpendwa, wazazi wetu wa kwanza walidanganywa na nyoka, wakaanguka
katika dhambi ya kwanza, wakapoteza utakatifu. Kukingiwa dhambi ya asili kwa Bikira
Maria, ni alama ya nguvu ya Mungu juu ya dhambi, dhambi ambayo iliwaangusha wazazi
wa Adamu na Eva. Kumbe kwa fundisho hili la imani tunaamini na kupata tumaini jipya
kuwa, kwa kuungana na Kristu dhambi na mwovu vimepatilizwa, havina nguvu tena ya kumshinda
mwanadamu. Hata hivyo lazima mwanadamu aungane na Kristo daima ndipo aweze kufaulu
mashindano hayo.
Mama Kanisa anasherehekea Siku hii kila tarehe 8 mwezi wa
kumi na mbili kila mwaka. Sherehe haitukuzi tu usafi na utakatifu wa Mama bali ni
fundisho la imani ambalo twapaswa kuliamini kina. Fundisho hili lilitangazwa na Baba
Mtakatifu Pio IX mnamo tarehe 8 Desemba mwaka 1854 na kuwekwa katika orodha ya mafundisho
sadikifu ya imani.
Mama Kanisa anaposherehekea sherehe hii anataka kila mmoja
wetu akumbuke mwanzo wa ukombozi wetu. Mama huyu alikingiwa dhambi ya asili ili aruhusu
Mwana wa Mungu kutungwa mimba katika mji usio na doa na hivi nasi katika utakatifu
huo tunaweza kukombolewa. Kwa hakika hatuwezi kukombolewa na awaye yote aliyeguswa
na doa la dhambi bali tunakombolewa na asiyeguswa na doa la dhambi naye ni Kristo
Mwana wa Mungu.
Mama Bikira Maria alizaliwa kama ambavyo Mungu alikuwa amekusudia
mwanadamu awe tangu mwanzo. Fikiria juu ya Adamu na Eva kabla ya kutenda dhambi yao
ya kwanza, walikuwa watakatifu na wakaharibu utakatifu wao kwa kiburi na tamaa ya
ulimwengu. Kinyume nao, Mama Maria anatunza utakatifu aliokabidhiwa katika neema ya
Mungu. Anakuwa tunda la kwanza la ukombozi. Anakuwa tabernakulo ya kwanza kumbeba
Mwana wa Mungu.
Mpendwa, kwa sherehe hii si tu tunakumbuka mwanzo wa ukombozi
wetu bali pia mwisho wa maisha yetu. Ndiyo kusema tunamwomba Mama atuombee tuweze
nasi kuonja matunda ya kazi ya Mwanae, tuweze kuishi bila dhambi tukilenga daima maisha
ya utakatifu. Mama huyu, ni mfano wa maisha bora, ni taa ambayo inaendelea kuwaka
anapojitokeza tena na tena katika maeneo mbalimbali akileta ujumbe wa Mwanae kwa mataifa.
Ombi kwako wewe unayenisikiliza na kutafakari pamoja nami, ebu jaribu kufanya safari
ya hija katika maeneo mbalimbali ambayo Mama Kanisa ameyaratibisha ukaonje mapendo
ya Mama wa Mungu na Kanisa.
Mpendwa tukiendelea kusali kwa kujitayarisha kwa
ajili ya Majilio, tunawakumbusha Waamini wote kuwa kama alivyojitoa kiaminifu Mama
huyu kuwa njia ya kupenya kwa Injili yaani Neno wa Mungu basi nasi katika mwaka huu
wa Maisha ya Wakfu tuweni daraja imara kwa ajili ya kupeleka Habari njema kwa mataifa.
Jambo hil pengine si rahisi kutekeleza, kumbe linahitaji neema za Mungu. Basi tunataka
kupeleka sala yetu kwa Mama huyu ili atuombee neema na msamaha toka kwa Mwanae.
Ni katika mantiki hiyohiyo ya sala tunawaombea wale wote waitwao Imakulatha wakashike
vema utauwa wao, wakamwite Mama Maria Bikira akawaimarishe katika utumishi wao kwa
umma na kwa Kanisa. Tunawaombea Masista wote wanaotimiza miaka 25, 50 ya utawa, wanaoweka
nadhiri za muda na za milele wakaimarishwe na Mama Bikira Maria Msaada wa Daima.
Tunaziombea
Parokia zote na mashirika yote ya kitawa waliojiweka chini ya ulinzi wa Mama Bikira
Mkingiwa wa dhambi ya asili wakaimarike na kuwa safina ya umoja, upendo na ustawi
wa kiroho na hasa katika maisha ya sakramenti. Tumsifu Yesu Kristu na Maria. Tafakari
hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.