2014-12-06 10:39:37

Kesheni na kusali!


Askofu mkuu Michele Pennisi wa Jimbo kuu la Monreale, Italia katika ujumbe wake kwa kipindi hiki cha Majilio anasema kwamba, huu ni wakati muafaka wa kuamsha tena matumaini miongoni mwa Wakristo, kwa ajili ya ujio wa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Ni wakati wa kuamsha uhai wa maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu, kwa kujikita katika toba, wongofu wa ndani na maisha ya Kisakramenti, ili kukumbatia utakatifu wa maisha unaonesha imani tendaji katika uhalisia wa maisha.

Ni mwaliko wa kuondokana na ubinafsi, chuki na uhasama pamoja na nafasi zote za dhambi, ili kumwandalia Masiha mioyo yenye amani, utulivu na kiasi. Lakini ikumbukwe kwamba, Mama Kanisa anaadhimisha Kipindi hiki cha Majilio kwa kutambua kwamba, Neno wa Mungu alikwishafanyika mwili na kuzaliwa duniani, yapata miaka elfu mbili iliyopita. Kanisa linaamini kwamba, Yesu atakuja tena kuwahumu wazima na wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho.

Majilio ni kipindi cha kukesha kwa njia ya Tafakari ya Neno la Mungu, Matendo ya Huruma, Maisha ya Sala na Utu wema, kila mtu akitambua dhamana na wajibu wake wa Kimissionari kwamba, anatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake pamoja na kuenzi shughuli na mikakati ya Uenezaji Injili kwa kuchangia kwa hali na mali.

Yesu Kristo atakapokuja tena, atawahukumu watu kwa kutumia kigezo cha upendo kwa Mungu na jirani, changamoto ya kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kutetea haki; kwa kumwilisha upendo pamoja na kutunza mazingira ambayo ni sehemu ya kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu kwa ajili ya mafao yake na kwa ajili ya kizazi kijacho!

Kipindi cha Majilio ni wakati wa sala na mshikamano na watu wanaoteseka kutokana na majanga mbali mbali yaani, vita, kinzani, maafa asilia na nyanyaso pamoja na madhulumu ya kidini kama inavyotokea huko Mashariki ya Kati. Wakristo wanaalikwa kuonesha mshikamano na watu wanaobaguliwa kutokana na rangi ya ngozi yao au mahali wanapotoka kwa kusahau kwamba, kila binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Waamini wasimamie haki zao msingi, utu na heshima yao.

Askofu mkuu Michele Pennisi anasema, Yesu Kristo anayesubiliwa katika Kipindi hiki cha Majilio kama cheche za matumaini, ndiye atakayekuja wakati wa utimilifu wa nyakati, changamoto ya kuendelea kukesha katika: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Matendo ya Huruma; kwa toba na wongofu wa ndani pamoja na kuchuchumilia utakatifu wa maisha, kwa kuwa ni mashahidi wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.