2014-12-05 14:59:49

Washirikisheni zaidi wanawake katika maisha na utume wa Kanisa


Tume ya Taalimungu Kimataifa ni matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ambamo Mababa wa Mtaguso waliitaka Vatican kuwa na Kikosi kazi cha wataalam wa kitaalimungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kutafakari na kufanya upembuzi yakinifu kuhusiana na masuala tete ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa, hasa yale yanayoleta mambo mapya, ili kulisaidia Kanisa katika azma yake ya kufundisha. Hadi sasa Tume hii imekwisha chapisha Nyaraka 27 ushuhuda makini wa majadiliano ya kitaalimungu.

Dhamana kubwa ya Tume hii ni kulisaidia Kanisa katika shughuli zake za maisha ya kiroho na kiakili, kwa kusikiliza kwa makini, dhamana ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameipatia kipaumbele cha kwanza wakati Ijumaa tarehe 5 Desemba 2014, alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Taalimungu Kimataifa, waliokuwa wanafanya mkutano wao wa mwaka mjini Vatican. Kanisa linapenda kusikiliza na kuhifadhi hazina hii moyoni mwa binadamu. Mwanataalimungu naye hana budi kusikiliza kwa makini sauti ya Roho Mtakatifu kwa kila anachotaka kuliambia Kanisa, kwa kusoma alama za nyakati ili kutoa tafsiri sahihi mintarafu hali ya nyakati hizi kwa kutumia mwanga wa Neno la Mungu.

Baba Mtakatifu anapenda kukazia umuhimu wa uwepo na ushiriki wa wanawake katika mchakato wa majadiliano ya kitaalimungu, kwani, Kanisa linatambua na kuthamini mchango wa wanawake katika maisha ya kijamii. Kumbe, wao pia wanaweza kutoa tafakari za kina katika masuala ya kitaalimungu kuhusiana na Fumbo la Yesu Kristo ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika. Baba Mtakatifu anawataka wanataalimungu kuhakikisha kwamba, wanatumia akili na imani ya wanawake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Tume hii inawaunganisha wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hali inayoonesha Ukatoliki wa Kanisa katika utofauti wake unaofumbata utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki, huku wakikazia umoja unaobubujika kutoka katika imani kwa Yesu Kristo na kurutubishwa na karama mbali mbali za Roho Mtakatifu. Kwa kuwa na mwelekeo kama huu, wajumbe wanaweza kupata mielekeo mbali mbali ya kitamaduni na taratibu katika utekelezaji wake pamoja na kuendeleza majadiliano ili kutajirishana na kukosoana pale inapobidi. Kazi za Tume hii zinaweza kuwa ni kielelezo cha ukuaji huu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Bikira Maria aliyekingiwa dhambi ya asili, aliweka mambo yote katika hazina ya moyo wake na kuyafanyia tafakari ya kina, ili kupata ukweli mkamilifu. Bikira Maria ni kielelezo makini cha Kanisa linalomngoja Yesu Kristo, ili akue na kuongezeka siku hadi siku katika imani kwa msaada na uvumilivu wa wanataalimungu. Bikira Maria ni mwalimu wa kweli wa taalimungu, awaombee na kuwadumisha katika upendo ili liweze kukua katika hekima na ufahamu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.