2014-12-05 12:13:24

Amani ni zawadi ya Mungu kwa njia ya Yesu Kristo!


Amani nawaachieni; amani yangu nawapa! Hii ndiyo kauli mbiu iliyoongoza mahubiri ya Kipindi cha Majilio yaliyotolewa na Padre Raniero Cantalamessa mhubiri wa nyumba ya Kipapa, Ijumaa tarehe 5 Desemba 2014 katika Kikanisa cha Mama wa Mkombozi, kilichoko mjini Vatican na kuhudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wakuu wa Kanisa. Amani ndiyo tema inayoongoza tafakari katika kipindi cha Majilio kwa Mwaka 2014, kwani vita bado inatishia usalama wa maisha na mali za watu na hivyo kuendelea kusababisha majanga na mateso makubwa.

Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo inayomwajibisha mwanadamu kudumisha mahusiano mema na Mwenyezi Mungu pamoja na kazi ya uumbaji. Kwa njia hii, binadamu anaweza kupata amani ya kweli na inayodumu, lakini amani hii inaweza kutoweka kama ndoto ya mchana ikiwa kama hakuna mahusiano mema na Mwenyezi Mungu na hapa ni mwanzo wa kinzani na migogoro ya kijamii.

Padre Cantalamessa anasema amani ni zawadi ambayo ni ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na imetekelezwa licha ya binadamu kuendelea kuogelea katika dimbwi la dhambi na mauti kwa kumkirimia zawadi ya Ukombozi ambayo maandalizi yake yanajionesha kwa namna ya pekee tangu Agano la Kale na kupata utimilifu wake kwenye Agano Jipya linalojikita katika amani. Hili ni Agano jipya na la milele, agano la amani linalowaelekea watu wote. Hii ni amani inayotolewa na Mwenyezi Mungu kwa wale wote anaowapenda.

Mitume walipokuwa wamejifungia kwa hofu na wasi wasi mkubwa, Yesu akawatokea na kuwaambia, "Shalom" Amani kwenu! Huu ni muhtasari wa kazi ya ukombozi, ndiyo maana Mama Kanisa kamwe hawezi kuchoka kutangaza amani duniani kwa kutambua kwamba, amani ni tunda la Msalaba wa Yesu, kwani wakishahesabiwa haki itokayo katika imani, waweze kuwa na amani kwa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Mateso na Kifo cha Yesu Kristo kimeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya mwanadanu, kwani amekombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Msalaba ni kielelezo cha msamaha na upatanisho kati ya Mungu na mwanadamu, kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu, Mwenyezi Mungu ameweza kuupatanisha ulimwengu wote pamoja naye. Amani ni zawadi ya Roho Mtakatifu ambayo Yesu Kristo mfufuka aliwapatia wafuasi wake, jioni ile walipokuwa wamejifungia ndani kwa woga wa Wayahudi; kumbe, amani ni zawadi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu; kwani Mungu ni amani, upendo na neema inayotolewa katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, mwaliko wa kujipatanisha na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.

Waamini wanahamasishwa kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kwa kuomba huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kumbe, upendo unapaswa kuheshimiwa na wala si kutwezwa, kwa kuimarisha mahusiano kati ya Mungu na binadamu kwa njia ya Yesu Kristo, ili kumwachia nafasi Roho Mtakatifu aweze kuleta mabadiliko yanayokusudiwa, kwani Mungu ni mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira bali mwingi a rehema na kweli, kiasi kwamba, mwanadamu anaweza kumwita Abba', yaani Baba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.