2014-12-04 14:53:55

Watakatifu wasionekana ni cheche za matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 4 Desemba 2014 amesema kwamba, kuna umati mkubwa wa watakatifu ambao wamefichika na wala hawaonekani; hawa ni wazazi, wagonjwa, watawa na Mapadre wanaomwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kwa kuwamegea wengine mapendo yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Ni umati wa watakatifu ambao umesimika maisha yao katika Neno la Mungu linalomwilishwa kila siku ya maisha, kiasi kwamba hawawezi kamwe kuteteleka katika maisha yao. Haitoshi kwa waamini kujisikia kuwa ni Wakristo au Wakatoliki, bali wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza utashi wa Mungu katika maisha yao, bila kujionesha kwani kishawishi kikubwa kwa watu wengi ni kupenda kuonekana mbele ya watu.

Baba Mtakatifu anasema, kuna umati mkubwa wa waamini ambao si lazima watangazwe na Mama Kanisa kuwa ni Watakatifu, lakini watakatifu wanaomwilisha upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao ya kila siku. Ni watu wanaotekeleza dhamana na utume wao katika familia pamoja na nyajibu mbali mbali walizokabidhiwa na Kanisa pamoja na jamii husika, daima wakionesha cheche za matumaini kutoka kwa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya tafakari ya kina ili kuangalia utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa, kwa waamini kuendelea kushikamana na Yesu Kristo. Anatambua uwepo wa dhambi na wadhambi ndani ya Kanisa, lakini hawa ni watu wanaotambua mapungufu yao na wako tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, ili kujenga maisha yao katika mwamba thabiti ambao ni Yesu Kristo.

Wale wanaojikweza na kujigamba, huku wakionesha Ukristo wao kwa nje, wataangushwa chini na Mwenyezi Mungu atawakweza maskini na wanyenyekevu wa moyo; wale ambao wanamwilisha Neno la Mungu katika maisha yao ya kila siku. Kipindi cha Majilio iwe ni fursa kwa waamini kujenga na kuimarisha maisha yao kwa Kristo ambaye ni mwamba thabiti, kwa kuweka matumaini yao kwake na kumkimbilia pae wanapoanguka dhambini ili kuonja tena huruma na upendo wake, kwa njia ya msamaha wa dhambi.

Waamini watambue kwamba, Yesu Kristo ni chemchemi ya furaha na matumaini; amani na mapendo; huruma na msamaha, changamoto ya kuweka matumaini katika Yesu, mwamba thabiti!







All the contents on this site are copyrighted ©.