2014-12-04 08:33:27

Uingereza na Vatican kwa pamoja zinataka kulinda na kudumisha amani, majadiliano na upatanisho!


Yesu Kristo anaendelea kuwaita na kuwatuma wafuasi wake kwenda sehemu mbali mbali za dunia ili kupeleka Habari Njema ya Wokovu inayojisimika katika misingi ya haki, amani na upatanisho, changamoto na mwaliko kwa Uingereza na Vatican kushirikiana kwa pamoja katika kuimarisha tunu hizi msingi kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatano tarehe 3 Desemba 2014 wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya Karne moja, tangu Uingereza na Vatican ziliporudisha tena mahusiano ya kidiplomasia. Ibada hii imefanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta za Roma na kuhudhuriwa na viongozi wa Kanisa na Serikali kutoka Uingereza na Vatican.

Kardinali Parolin katika mahubiri yake amezitaka nchi hizi mbili kuendelea kushirikiana kwa dhati ili kulinda na kutetea wanyonge kama ilivyokuwa wakati wa Vita kuu ya kwanza na ya Pili ya Dunia na kama hali inavyojionesha kwa sasa. Wawe ni wadau wakuu katika kuhamasisha mchakato wa majadiliano ya upatanisho kati ya watu, ili kujenga na kuimarisha haki na amani miongoni mwa jamii ya binadamu pamoja na kuendelea kutoa msaada wa hali na mali kwa watu wanaokumbwa na maafa na majanga asilia sehemu mbali mbali za dunia.

Hii ni changamoto pia ya kukumbatia na kuenzi Injili ya Uhai kwa kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kukataa kishawishi cha kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo unaojikita katika sera za kifo laini, biashara haramu ya binadamu pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Kardinali Parolin amepongeza juhudi zinazofanywa na nchi hizi mbili kwa kuzingatia tunu msingi za maisha ya Kikristo na kimaadili sanjari na mchakato wa majadiliano ya kiekumene unaotekelezwa na Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa umoja wa Wakristo, ingawa bado kuna madonda makubwa ya utengano huu yanayoapaswa kufanyiwa kazi, ili kupata tiba muafaka.

Kardinali Parolin anasema, maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kipindi cha Karne moja tangu Vatican na Uingereza viliporudisha mahusiano ya kidiplomasia ni kielelezo kwamba, imani imekuwa ni msingi katika mchakato wa majadiliano baina ya pande hizi mbili. Wakristo bado wanahamasishwa kutoka kifua mbele kwenda ulimwenguni ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu; dhamana inayowahitaji watu wanaojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Waamini wajitahidi kusoma, kulisikiliza, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu, ilikuzima njaa na kiu ya Neno la Mungu katika maisha ya watu. Watu wana kiu ya ukweli na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kardinali Parolin amekumbusha kwamba, katika kipindi cha miaka mingi kupita, Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1982 alithubutu kutembelea Uingereza na baadaye, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipokwenda Uingereza ili kumtangaza Kardinali John Henry Newman kuwa Mwenyeheri. Malkia Elizabeth wa Uingereza alimtembelea Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican tarehe 3 Aprili 2014.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Uingereza uliingiwa na mchanga kwa muda wa miaka 340 hadi ilipogota tarehe 7 Desemba 1914, nchi hizi mbili zikarudisha tena uhusiano wao wa kidiplomasia. Kweli ni rahisi kuvuruga mahusiano ya kidiplomasia, lakini kuyarudisha tena, itachukua miaka mingi.

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.