2014-12-04 15:21:25

Tanzania yapata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Saudia!


Serikali ya Tanzania imewekeana sahihi mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa zaidi ya shilingi bilioni 45.2 na Shirika la Maendeleo la Saudia kwa lengo la kuboresha miradi wa maji kwa wilaya ya Same, Mwanga na ujenzi na ukarabati wa barabara Visiwani Zanzibar. Mkataba huo umesainiwa Alhamisi, tarehe 4 Desemba 2014 Jijini Dar es salaam na Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Saudia Mhandisi Hassan Al-Attas.

Akiongea na waandishi wa habari katika hafla hiyo, Waziri Saada amesema kuwa kati ya mkopo huo shilingi bilioni 41.25 ambazo ni sawa na Dola za Kimarekani milioni 25 zitagharimia mradi wa maji katika wilaya za Same na Mwanga na shilingi bilioni 3.96 kwa ajili ya maradi wa barabara Pemba, visiwani Zanzibar.

Waziri Saada alilishukuru Shirika la Maendeleo la Saudia kwa jitihada zao za kuisaidia Serikali ya Tanzania katika kautatua tatizo la maji wilaya za Same na Mwanga pamoja na uboreshaji wa barabara katika visiwa vya Pemba. Aidha, mradi wa maji wa Same- Mwanga utagharimu Dola za Kimarekani milioni 110.34 ambazo benki ya BADEA, Shirika la Maendeleo Kuweit, OPEC na mashirika mengine wamekubali kukamilisha sehemu ya fedha iliyobakia.

Mradi wa maji wa Same - Mwanga baada ya kukamilika utasaidia kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji vijijini amabapo utasaida kuboresha hali ya maisha wa wananchi wa maeneo hayo, upatikanaji nwa maji safi na salama kwa maendeleo ya afya za wakazi hao na kuboresha uchumi wao kwa kutumia muda mwingi kwa shuighuli za uzalishaji mali badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Saudia Mhandisi Hassan Al-Attas amesema kuwa makataba waliosaini leo unaonesha kuwa Saudi Arabia iko mstari wa mbele katika kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi wake kwa kuzingatia mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizo. Hafla hiyo ilihudhuriwa waandishi wa habari na baadhi ya watumishi wa wizara ya Fedha na wawakilishi wa Serikali ya Saudi Arabia.








All the contents on this site are copyrighted ©.