Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Galles limejiwekea mikakati ya kichungaji
kwa ajili ya Kipindi cha Majilio, ili kuwahamasisha waamini kusoma, kusikiliza, kutafakari
na kulitangaza Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao.
Kwa namna
ya pekee, mkazo umewekwa tarehe 7 Desemba 2014, Jumapili ya pili ya Kipindi cha Majilio,
kipindi cha matumaini, wakati ambapo waamini wanasubiri kwa hamu kubwa kuzaliwa kwa
Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu.
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican
waliwahimiza waamini kujikita katika kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la
Mungu katika uhalisia wa maisha yao kama kielelezo cha imani tendaji, kwani Kristo
ni utimilifu wa ufunuo wa Mungu kwa watu wake. Ni wajibu na dhamana ya Kanisa kuhakikisha
kwamba, inawarithisha waamini utajiri wa Neno la Mungu, kwa kufuata Mapokeo Matakatifu
kwa kutambua kwamba, Biblia Takatifu imeandikwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, kwa
kumshirikisha mwanadamu hekima ya Kimungu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza
linasema kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wa Kitume, Neno
la Mungu, “Verbum domini” anawaalika waamini kusoma Neno la Mungu kwa umakini mkubwa
bila ya kuchoka, kwani kwa njia hii, wataweza kumfahamu Yesu Kristo sanjari na kukabiliana
na changamoto za maisha kwa msaada wa Neno la Mungu.
Waamini wanakumbushwa
kwamba, kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo, Waamini walisome Neno la Mungu
kwa furaha na uchaji mkubwa pamoja na kujiundia mazingira ya sala, ili Mwenyezi Mungu
na binadamu waweze kuongea kwa pamoja, kwani wanaongea na Mungu wakati wa sala au
wanaposikiliza kwa makini Neno la Mungu likitangazwa mbele yao.
Jumapili ya
Neno la Mungu ni mwaliko na changamoto kwa Waamini kuvumbua mbinu mpya inayobubujika
kutoka kwenye Neno la Mungu, ili kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa
kujikita katika Neno la Mungu. Lengo ni kuinjilisha na kuimarisha Katekesi, ili waamini
waweze kukiri Imani, Kuiadhimisha, Kuimwilisha na Kuisali.
Baraza la Maaskofu
Katoliki Uingereza na Galles, kwa kushirikiana na Chama cha Biblia Uingereza wanasema
kwamba kipindi cha Majilio ni wakati muafaka wa kungojea kuzaliwa kwa Masiha, ni wakati
wa kukesha kwa Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma. Waamini wanahimizwa
kukuza na kujenga moyo wa kusoma, kusikiliza, kutafakari, kutangaza na kumwilisha
Neno la Mungu katika uhalia wa maisha yao ya kila siku!
Na Padre Richard A.
Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.