Mikakati ya maendeleo itoe kipaumbele cha kwanza katika kupambana na umaskini, njaa
na lishe duni!
Umoja wa Mataifa ni jukwaa ambalo watu wasiokuwa na sauti wanaweza kusikilizwa kwa
heshima na taadhima, ili kuibua mbinu mkakati utakaofanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa
mara baada ya kukamilika kwa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015.
Mikakati ya maendeleo itakayofuatia, haina budi kupata ridhaa ya wanachama
wengi kutoka Jumuiya ya Kimataifa, bila shuruti ya aina yoyote ile na kwamba, kuna
haja ya kutafuta ushauri mpana zaidi, ili kweli Jumuiya ya Kimataifa iweze kupata
mafanikio makubwa zaidi katika mikakati ya maendeleo endelevu. Hapa kuna haja ya kufanya
upembuzi yakinifu kwa kupima mafanikio, matatizo na changamoto zitakazokuwa zinajitokeza
katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo baada ya mwaka 2015.
Ni changamoto
ambayo imetolewa na Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye
Umoja wa Mataifa, wakati akichangia hoja kwenye kikao cha sitini na tisa cha Baraza
kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu mikakati ya maendeleo mara baada ya mwaka 2015. Anasema
vielelezo vinavyotolewa havina budi kuchambuliwa kwa umakini mkubwa ili kuangalia
kama vinatekelezeka kutokana na utofauti mkubwa unaojionesha kati ya nchi wanachama
wa Umoja wa Mataifa.
Askofu mkuu Auza anasema, kipaumbele cha kwanza kiwe ni
kupambana na umaskini, baa la njaa na utapiamlo mambo ambayo bado yanasababisha majanga
makubwa kwa wananchi wengi wanaoishi katika Nchi zinazoendelea duniani, kwani huu
ni wajibu wa kimaadili kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa kama alivyokazia Baba Mtakatifu
Francisko alipokuwa anazungumza na wajumbe wa mkutano wa FAO hivi karibuni mjini Roma.
Utekelezaji wa mikakati hii uwe ni mwendelezo wa mafanikio yaliyopatikana
siku za nyuma, kwa kuweka masuala ya ushauri katika mfuko wa maendeleo wakati ambapo
mikakati ya maendeleo endelevu iunganishwe katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Ujumbe wa Vatican unatarajia kuendelea kushiriki kikamilifu katika mikutano mikuu
itakayofanyika hapo mwakani pamoja na ule unaotarajiwa kuwakutanisha wakuu wa Nchi
na Serikali mwezi Septemba, 2015.