2014-12-04 09:50:21

Huo ni mwanzo tu, Picha kamili iko njiani! Upele umempata mkunaji!


Leo habari imeanza kuandikwa hivi: “Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.” Mwandishi mahiri hawezi kuanza kuandika habari yake namna hiyo, kwa mfano: “Sasa ninaanza kuandika habari yangu.” Kumbe, ukitafakari kwa kina, mwanzo huo unao ujumbe mzito sana. Ili tuweze kupata ujumbe toka sehemu ya Injili ya leo tujaribu kufuatilia kwa kina maana ya lugha iliyotumika.

“Mwanzo”: Neno la kwanza tunalokutana nalo ni “Mwanzo”. Namna ya hii ya kuanza kuandika imetumika pia na mwandishi wa kitabu cha Mwanzo cha Biblia Agano la kale akilitumia neno la kiebrania Bereshit. “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi” Mwa. 1:1). Huo ulikuwa ni mwanzo wa uumbaji wa ulimwengu wa kale. Injili ya Marko ni ya kwanza kuandikwa mwaka wa 68, yaani miaka 38 baada ya kufa na kufufuka Kristu.

Katika ulimwengu wa wakati huo wa warumi na wagiriki, kulikuwa tayari na vikundi mbalimbali vya wafuasi wa Kristu na baadhi ya mitume walikuwa wamekufa tayari wakishuhudia maisha ya Kristu, kama vile akina Petro na Pauli wakati wa madhulumu ya Nero. Kwa hiyo jumuia za Kristu zilikuwa karibu ni za kizazi cha pili au cha tatu cha mitume. Wakristu bado walikuwa wanashuhudia katika ulimwengu uonevu na madhulumu, ukatili na vita. Wakawa wanajiuliza, “Ulimwengu huu mpya wa ukristu ulianzaje?” Kwa hiyo Marko anajitosa kueleza jinsi mambo hayo yalivyoanza na Yohane Mbatizaji. Huyo alikuwa akihubiri kando ya mto Yordani na kuwabatiza watu. Hata Yesu alienda mto Yordani ili kubatizwa naye. Hivyo ndivyo ilivyoanza hiyo Habari Njema.

Kisha linafuata neno Injili. Neno hilo Injili halina maana ya mwanzo wa kitabu, la hasha bali ni mwanzo wa “Tangazo la furaha, tangazo la sikukuu. Habari njema, inayoleta furaha.” kwa wote wanaoishi katika giza na kivuli cha vitisho vya mauti. Habari hii ni muhimu hata kwa Marko mwenyewe, kwani wakati anaandika mwaka wa 68 huko Roma hali ya kisiasa ilikuwa tete sana hasa ikizingatiwa kulikuwa na vita vya ndani vya nchi vinavyoendelea, aidha, hadi wakati huo kulikuwa taya kumetokea tayari falme za kikaisari karibu kumi na mbili, na kati yao, makaisari nane walikuwa wameuawa kikatili.

Kati ya tawala hizo, ule ufalme wa Augusto Oktaviani, ndiyo ulioonekana kuleta amani na maendeleo ya kijamii. Kuzaliwa kwake kulikuwa tarehe 23 mwezi wa tisa. Huko kuzaliwa kwake warumi walikuchukulia kuwa kama ndiyo mwanzo wa maisha mema kwa kila Mrumi. Kwa hiyo wakaipanga tarehe hiyo iwe mwanzo wa mwaka badala ya mwezi Januari kama ilivyo sasa. Marko aliyeishi miaka hamsini baadaye alijua kwamba hata huko kuzaliwa kwa Augusto Oktaviano kulikoishapita, na matatizo yalikuwa bado palepale yanaendelea. Kwa hiyo kuzaliwa huko hakukuwa tena na sera ile ya mwanzo mpya wa maisha mema ya furaha.

Marko anatumia lugha hiyo hiyo ya mwanzo wa Mwaka wa Furaha, anapotaka kuandika mwanzo mpya wa Habari njema ya furaha ya ujio wa Yesu Kristu aliye Habari Njema ya kweli.

Kisha yanayofuata maneno mazito, yaani: “Yesu Kristo, Mwana wa Mungu”. Neno Kristo au Masiha, maana yake ni mpakwa wa Bwana. Katika Agano la Kale mpakwa huyo alipata nguvu ya kimungu, aliweza kufanya mambo ya kimungu na kuubadilisha ulimwengu. Yesu ndiye huyo mpakwa wa Mungu. Huyu ndiye anayeweza kuubadilisha ulimwengu huu. Na “Mwana wa Mungu”. Katika utamaduni wa wayahudi, “Mwana” ilimaanisha kufanana kabisa na mzazi, siyo tu sura bali katika kuishi na kutenda mambo.

Kwa hiyo Mwana wa Mungu ni yule anayefanana kabisa na Mungu. Hapa angalia jinsi Yesu anavyofanana na Mungu. Anavyozunguka na kupita katika kila mazingira ya watu ili kuinadisha sura hiyo ya Mungu. Mungu amefika kujionesha alivyo katika Mwanae Yesu Kristu.

Halafu yanafuata maneno haya “Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya: ‘Tazama, namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako atakayeitengeneza njia yako.’” Lugha hiyo ya Nabii Isaya, inatekelezwa na nabii Yohane. Huyu ndiye anayetimiza unabii huo. Yohane ndiye atakayeiandaa njia hiyo, yaani Yesu Kristo. Kwa kuipitia njia hiyo tunaweza kwenda kwa Baba. Njia hiyo yabidi kuiandaa.

Yohane anawaalika wote kujiandaa, kujiweka sawa, kuwa safi, kuandaa kupita katika barabara hiyo. “Itengenezeni njia ya Bwana yanyosheni mapito yake.” Yohane aliwaweka watu sawa akihubiri ubatizo wa toba iletayo ondoleo la dhambi na kuwabatiza. Akawataka watu waongoke wawe na namna mpya ya kufikiri, ya kutenda. Kubadili fikra juu ya Mungu wa Agano la kale, aliyekuwa mkali, anayelipiza kisasi, nk. Bila kubadili fikra hiyo huwezi kuingia na kuifuata barabara hii mpya ya Mungu mwema, mwenye rehema, mwenye kutenda haki kwa wote.

Aidha, “Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao.” Sentensi hii itaeleweka tu endapo tukifahamu umuhimu wa mto Yordano kwa Wayahudi. Mto Yordano ndiyo waliovuka wayahudi wakitokea utumwani na kuingia katika nchi yao huru. Hivi mto Yordani ulikuwa ni mpaka kati ya nchi ya kipagani au nchi ya utumwa na nchi huru ya wayahudi.

Mwinjili Marko anatuambia kwamba watu walitoka uyahudini na Yerusalemu. Maana yake watu hao ni Wayahudi waliokuwa tayari katika nchi huru. Sasa lakini watu hao wanamwendea Yohane aliyekuwa upande wa pili wa mto ili wabatizwe na kuingia tena katika nchi huru. Hapa yaonekana watu hao walikwua bado wapagani na watumwa ingawa walikuwa katika nchi huru.

Ni sawa na nchi iliyopata uhuru toka utawala wa mkoloni, lakini inaendelea bado kuteseka chini ya ukoloni mambo leo wa viongozi wao. Hivi wayahudi hawa na wote wa kutoka Yerusalemu iliwabidi wabatizwe upya. Baada ya ubatizo huo ndipo Yohane angeweza kuwakabidhi kwa Musa mpya yaani Yesu Masiha, atakayewaingiza katika ardhi ya kweli kwenye ulimwengu mpya wa Heri. Kwa hiyo wakafika kubatizwa naye wakiziungama dhambi zao.

Kisha tunaelezwa mvao na lishe ya huyo Yohane Mbatizaji kwamba “alikuwa amevaa singa (nywele) za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu.”

Taarifa hizi si za kihistoria unazoweza kuzibainisha, bali ni lugha ya picha inayoeleza jinsi alivyokuwa anavaa na kula nabii yeyote wa kiyahudi. Kwa hiyo kuhusu mvao wa Yohane ulikuwa ni ule wa Manabii wote wa kale yaani nywele za ngamia na kujifunga mshipi wa ngozi kiunoni. Kadhalika namna ya kula yaani nzige na asali ya mwitu, haikumaanisha kuishi maisha ya kujitesa, la hasha. Hivyo vilikuwa ni vyakula vitamu na vyenye vitamini.

Nzige tungeweza kuzifananisha na jinsi zinavyoshabikiwa senene au kumbikumbi au ivishimu kwa baadhi ya makabila. Kwa kawaida chakula hicho kilikuwa ni uhondo waa watu wa jangwani. Kadhalika asali ni tamu sana. Tunaoizungumzia juu ya jangwa maana yake ni matatizo yak ila aina.m mathalani, kukosa mambo muhimu ya maisha hasahasa kukosekana maji, chakula, vitu vinavyolinganishwa na kukoseana haki, wivu, udhulumu, kukosa uhuru nk. Kwa hiyo kupita humo na kutoka maana yake kuachana na shuruba za jangwa na kuingia katika nchi huru. Kwa hiyo sasa kutakuwa na Musa mpya. Yohane ndiye Nabii anayemwandaa huyo Musa.

“Mimi ninabatiza kwa maji, bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu”. Maana yake, ubatizo wa Yohane ni wa nje, yaani ni wa kuvuka tu mto Yordani toka mashariki kuvukia magharibi. Hayo ni maji yanayosafisha nje tu. Kumbe ubatizo wa kikristu siyo wa nje, bali ni wa kiroho. Ubatizo huo mpya unaleta maisha mapya ya kutoka hali ya uovu, ya utumwa na kumwingiza mtu kwenye roho mpya. Kwa hiyo, mwito wa Injili ya leo kwetu ni kujiandaa kumpokea huyo Musa mpya atakayetufanya huru wa kweli.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.