2014-12-03 08:05:07

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio Mwaka B wa Kanisa


Mpendwa mwana wa Mungu ninakualika katika tafakari ya Neno la Mungu ili polepole ukaze mwendo katika maandalizi ya kumpokea Mwana wa Mungu. Ni Dominika ya pili ya majilio. RealAudioMP3

Dominika ya kwanza tuliweka bayana nini wajibu wako katika kipindi cha majilio. Ni kukaa tayari kwa kulitafakati Neno la Mungu, kupokea sakramenti na kutenda yote yaliyo mema daima. Tuliweka mbele yako watu wanne ambao katika matayarisho ya ujio wa Bwana wanahusika moja kwa moja, nao ni Nabii Isaya, Yohane Mbatizaji, Mtakatifu Yosefu na Mama Bikira Maria mama wa Mungu. Katika Dominika ya pili Neno linatualika KUONGOKA NA KUANZA MAISHA MAPYA.

Katika somo la kwanza nabii Isaya anawaalika wana wa Israeli ambao bado wako utumwani Babeli kuwa na utulivu kwa kuwa ukombozi wao unakaribia. Wameteseka na kujuta na hivi Bwana amesikia kilio chao. Nabii Isaya anaimba wimbo akiwaambia Waisraeli wakatengeneze njia ya Bwana, wakanyoshe mapito yake na wakasawazishe milima na mabonde. Yote haya Nabii Isaya, anawataka wasawazishe mioyo yao ili Bwana apate kuingia ndani mwao. Kwa hakika anawaambia yule ajaye ni mkuu ambaye kwake yeye utukufu wa Bwana utafunuliwa. Wote wanaalikwa kutangaza habari hiyo njema ya furaha juu ya milima na miji ya Israeli. Mafundisho haya ni kwa ajili yetu hivi leo tukayashike na yatupe nguvu, ndiyo kujiandaa vema kumpokea Masiya, tukitangaza habari ya ukombozi na furaha katika miji yetu na vijiji vyetu, ikibidi hata tukitokea milimani.

Mtakatifu Petro katika somo la pili anakazia ujumbe wa maandalizi akisema, katika kusubiri jambo la msingi si kujua siku wala saa bali kukaa tayari kama askari alindavyo mlango na asubirivyo kupambazuke. Bwana hakawii kutimiza ahadi yake ya kuja lakini atakuja siku ambayo hatujui. Pamoja na hili Bwana hapendi hata mmoja apotee bali apokee toba. Kumbe majilio ni kipindi cha toba, ni kipindi cha msamaha kwa wakosefu, ni kipindi cha kupanda mazao kwa ajili ya mavuno mazuri ndio ujio wa Masiya. Kumbe mwaliko wa Mtakatifu Petro ni wa kweli yaani kutubu na kuongoka ili kujenga tabia ya utakatifu, mwaliko kwa wote.

Mwinjili Marko anarudia ujumbe uleule wa Nabii Isaya, yaani anakazia matayarisho kina ya njia ya Bwana. Anataka kila mmoja wetu aondoe milima na mabonde katika njia atakayopita Bwana. Nabii Yohane Mbatizaji ni kielelezo cha maandalizi hayo anapowaalika watu wakaondoe vichaka na manyasi yasiyohitajika katika barabara ambayo ni mapito ya Masiya. Kwa hakika barabara hii ni maisha ya kiroho, ni moyo wako, ni maisha yako katika ujumla wake. Ni lazima maisha yetu yawe ni maisha ya kumpendeza Mungu yaani bila maotea ya magugu katika shamba la ngano.

Ujio wa Masiya unaambatana na kuunda taifa jipya na hivi unadai kukazia utayari katika maisha ya toba, maisha ya kumpendeza Mungu na watu, maisha ambayo huruhusu mishumaa tuliyotaja katika Dominika ya kwanza iendelee kuwaka mpaka Bwana atakapokuja. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.