Watawa mnachangamotishwa kushiriki kikamilifu katika maisha ya Jumuiya ndogo ndogo
za Kikristo!
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka kuhusu Fumbo la Kanisa, Yaani
"Lumen gentium", Mwanga wa Mataifa, wanawahamasisha watawa popote pale walipo kulidhihirisha
Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yanayojikita katika tafakari ya Neno la
Mungu, Sala na Matendo ya huruma, kama kielelezo hai cha uwepo wa Mungu kati ya watu
wake. Kwa njia ya uaminifu na udumifu katika wito na maisha yao ya kitawa, wanaendelea
kumpamba Bibiarusi wa Kristo, yaani Kanisa kwa kuwahudumia watu kwa njia ya majitoleo
na moyo mkuu.
Watawa watambue
kwamba, changamoto ya kuchuchumilia utakatifu wa maisha inapata chimbuko lake kutoka
katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mwaka wa Watawa Duniani uliozinduliwa katika Maadhimisho
ya Jumapili ya kwanza ya kipindi cha Majilio, ili ni fursa kwa watawa sehemu mbali
mbali za dunia kuupamba ulimwengu kwa njia ya harufu ya utakatifu wao unaojidhihirisha
katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja maisha
ya kijumuiya yanayofumbata umoja, udugu na mshikamano wa dhati.
Askofu mkuu
Josephat Lpuis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania katika mahojiano maalum na
Radio Vatican wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani anasema
kwamba, watawa wanapaswa kutambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume
wa Kanisa. Miito mbali mbali ya watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume inapata
asili na utimilifu wake ndani ya Kanisa.
Hii ni changamoto kwa watawa kuhakikisha
kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Makanisa mahalia bila ya
kuingia katika kishawishi cha kujitafuta wenyewe, kwa kujiweka pembeni mwa mikakati
ya shughuli za kichungaji inayotolewa na Makanisa mahalia.
Askofu mkuu Lebulu
anawataka watawa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kushikamana
na Familia ya Mungu katika ujumla wake, ili yote yafanyike kwa sifa na utukufu wa
Mungu na mwanadamu aweze kukombolewa na kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu kwa waja
wake. Watawa wanayo nafasi na wajibu mkubwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia,
kumbe, watawa hawapaswi kujisikia kuwa ni wageni katika utekelezaji wa mikakati ya
shughuli za kichungaji kwani wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa.
Askofu
mkuu Lebulu anasema, Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, iwe ni fursa ya kutafakari
na kumwilisha mashauri ya Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watawa; kwa kujikita
katika Ufukara wa Kiinjili kwa njia ya maneno lakini zaidi kwa ushuhuda wa matendo
yao; Utii wa Kiinjili unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake pamoja
na kukazia Usafi kamili, kielelezo cha sadaka na majitoleo makubwa kwa ajili ya Mungu
na jirani. Watawa washiriki kikamilifu katika maisha ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo
ili waweze kuwasaidia waamini kulitafakari vyema Neno la Mungu na kulitolea ushuhuda
kwa njia ya imani tendaji.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican.