Mtu mnyenyekevu anauwezo wa kumfahamu Mungu na taalimungu inafanyika kwa njia ya sala
na tafakari!
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha,
kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 2 Desemba 2014 amewataka wale wote wanaojifunza
taalimungu, kuifanya shughuli hii kwa kupiga magoti, moyo mkuu na unyenyekevu, kwani
imependeza Mwenyezi Mungu kujifunua kwa watu wanyenyekevu kama walivyo watoto wadogo,
na kamwe wasitegemea akili zao wenyewe, vinginevyo watashindwa kulifahamu Fumbo la
Maisha ya Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, Ufalme wa Mungu ulioanzishwa
na Yesu Kristo mwenyewe ni kwa ajili ya maskini wa roho kama anavyofundisha Mwinjili
Luka, ndiyo maana Yesu anamshukuru Baba yake wa mbinguni kwa kuyaficha mambo haya
na kuwafunulia watoto wadogo, kwani ndivyo ilivyompendeza, mwaliko kwa Wakristo kujenga
na kukuza moyo wa unyenyekevu, kwa njia ya sala na tafakari ya kina.
Umaskini
wa roho ni udongo mzuri kwa ajili ya kutafakari Fumbo la Utatu Mtakatifu. Yesu anajifunua
si kama nahodha, kiongozi mwenye nguvu na madaraka makubwa au jemedari wa vita bali
kama mche mwororo, mpole na mnyenyekevu wa moyo. Yesu anakuja kumkomboa mwanadamu
kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili kumshirikisha ile furaha ya uzima wa milele.
Anakuja kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu, wagonjwa, maskini na wale wote wanaodhulumiwa
na kunyanyaswa.
Ukuu wa Fumbo la Maisha ya Mungu unaweza kufahamika anasema
Baba Mtakatifu kwa njia ya Yesu Kristo, aliyejinyenyekesha, hata kufa Msalabani, nje
ya Yesu ni vigumu sana kuweza kumfahamu Mwenyezi Mungu. Kipindi cha Majilio, iwe ni
fursa kwa waamini kumkaribia zaidi Mwenyezi Mungu na kutembea pamoja naye katika hali
ya unyenyekevu, upole na umaskini, kwa kujisikia kuwa ni wadhambi wanaohitaji kuonja
huruma na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yesu anakuja ili kumkomboa mwanadamu!