Yaliyojadiliwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!
Ifuatayo ni hotuba ya Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo P. Pinda (MB), wakati wa kuhitimisha
shughuli za Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe
29 novemba, 2014.
I: UTANGULIZI a) Masuala ya jumla Mheshimiwa Spika,
Leo
tunahitimisha shughuli za Mkutano wa Kumi na Sita na Kumi na Saba wa Bunge lako Tukufu.
Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama
siku ya leo.
Mheshimiwa Spika, 2. Mkutano huu ulijumuisha kujadili kazi
kubwa zifuatazo: Kwanza: Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka
2015/2016; Pili: Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa Mwaka 2014 [The Tax
Administration Bill, 2014]; Tatu: Muswada wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
wa Mwaka 2014 [The Value Added Tax Bill, 2014]; Nne: Muswada wa Marekebisho ya
Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2014 [The Public Private
Partnership (Amendment) Bill, 2014]; na Tano: Muswada wa Sheria ya Marekebisho
ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2014, [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill,
2014]. Aidha, ni hivi mapema leo Miswada 11 ya Sheria ya Serikali kuhusu mambo
mbalimbali ilisomwa kwa mara ya kwanza.
Mheshimiwa Spika, 3. Nitumie nafasi
hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika Kamati ya Mipango hapa
Bungeni kwa kujadili kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa na Serikali kuhusu Mpango
wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2015/2016. Maoni na Ushauri tuliopokea kutoka kwa Waheshimiwa
Wabunge tutauzingatia wakati wa maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2015/2016. Vilevile,
niwashukuru kwa kujadili na kupitisha Miswada ya Sheria niliyoitaja hivi punde. b)
Maswali
Mheshimiwa Spika, 4. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata
fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya Papo Papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Jumla ya maswali 241 ya msingi na 662 ya nyongeza yameulizwa na Waheshimiwa Wabunge
na kujibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 18 ya msingi na 13 ya nyongeza yaliulizwa
na kujibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
c) Kauli
za Mawaziri, Mheshimiwa Spika,
5. Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa tarehe
17 Novemba, 2014 nilipata fursa ya kutoa Kauli ya Serikali kuhusu Mgogoro kati ya
Wakulima na Wafugaji Wilayani Kiteto. Aidha, baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri walipata
nafasi ya kutoa Kauli mbalimbali za Serikali kama ifuatavyo:
i) Kauli ya Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu taarifa zilizotolewa na Vyombo
vya Habari za shutuma dhidi ya Serikali za China na Tanzania kujihusisha na Biashara
Haramu ya Pembe za Ndovu na ile inayohusu Kuridhia Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu
Demokrasia, Uchaguzi na Utawala wa Mwaka 2007; ii) Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii kuhusu Hali ya Dawa Nchini na Matibabu ya Saratani Nchini; na iii) Kauli
ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika kuhusu Mwenendo wa Soko la Nafaka na Mpango
wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo.
Maazimio Mheshimiwa Spika, 6. Tarehe
7 Novemba, 2014 Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili na kupitisha Azimio
la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Anne Semamba Makinda (Mb.), Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mabunge ya Nchi Wanachama wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-PF). Aidha, katika Mkutano huu Waheshimiwa
Wabunge walipata pia fursa ya kujadili na kuridhia
Maazimio mengine yafuatayo:
i)
Azimio la Bunge kuhusu Itifaki ya Kuanzishwa kwa Tume ya Utafiti wa Afya, Jumuiya
ya Afrika Mashariki; ii) Azimio la Bunge la Kufuta na Kusamehe Madai au Hasara
itokanayo na Upotevu wa Fedha na Vifaa vya Serikali kwa Kipindi Kilichoishia tarehe
30 Juni, 2011; iii) Azimio la Bunge la kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
kuhusu Ushirikiano katika Masuala ya Kiulinzi [The East African Protocol on Cooperation
in Defence Affairs]; na iv) Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Uzuiaji wa Vitendo
Haramu dhidi ya Usalama wa Miundombinu ya Kudumu iliyojengwa chini ya Bahari katika
Mwambao wa Bara ya Mwaka 1988 [The Protocol for the Suppression of Unlawful Acts Against
the Safety of Fixed Platforms located on the Continental Shelf – SUA, 1988].
e)
Taarifa Maalum za Kamati Mheshimiwa Spika, 7. Mwisho, lakini siyo kwa umuhimu,
Waheshimiwa Wabunge walipokea Taarifa Maalum ya Kamati ya Hesabu za Serikali (Public
Accounts Committee - PAC) Kuhusiana na Miamala iliyofanyika katika Akaunti ya “ESCROW”
ya TEGETA pamoja na umiliki wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Mheshimiwa
Spika, 8. Naomba nitumie fursa hii, kwanza kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kwa
kuruhusu Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwasilisha Taarifa hii Maalum kwenye
Bunge lako Tukufu kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. Aidha, niwashukuru Mwenyekiti na
Wajumbe wote wa Kamati kwa uchambuzi wao wa kina na Mapendekezo yao kama yalivyowasilishwa
katika Mkutano huu. Nitumie fursa hii pia kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri waliozungumza
kwa niaba ya Serikali nzima kutoa maelezo yaliyolenga kutoa ufafanuzi wa hali halisi
ya suala hili la Akaunti ya ESCROW ya TEGETA na pia kujibu baadhi ya Hoja za Kamati.
UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA a) Maandalizi ya Kupiga Kura tarehe 14 Desemba,
2014 Mheshimiwa Spika, 9. Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa Tanzania
Bara unatarajiwa kufanyika tarehe 14 Desemba, 2014. Uchaguzi huo ni wa kawaida na
unahusisha Uchaguzi wa Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji, Mitaa, Wajumbe wa Halmashauri
za Vijiji na Wajumbe wa Kamati za Mitaa. Taarifa nilizonazo ni kwamba hadi sasa maandalizi
ya Msingi kuwezesha Uchaguzi huo kufanyika yamekamilika.
Mheshimiwa Spika,
10. Ili kuhakikisha kuwa Uchaguzi huo unafanikiwa, maandalizi ya Kanuni za Uchaguzi
yalifanyika kupitia Vikao vya Wadau mbalimbali ili kupata maoni, mapendekezo na ushauri
ambao umesaidia katika kuboresha Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Wadau walioshirikishwa
ni pamoja na Viongozi wa Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa Kudumu; Makatibu Tawala
wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Asasi Zisizo za Kiserikali
(AZAKI).
b) Uandaaji wa Kanuni za Uchaguzi za Mwaka 2014 Mheshimiwa Spika, 11.
Katika maandalizi ya awali, orodha ya Vijiji, Mitaa na Vitongoji iliandaliwa na kuchapishwa
katika Gazeti la Serikali la tarehe 22 Agosti, 2014 lenye Tangazo la Serikali Namba
300 kwa Halmashauri za Miji na Tangazo Namba 301kwa Halmashauri za Wilaya. Orodha
hiyo imejumuisha Kata, Vijiji na Mitaa. Katika Uchaguzi wa mwaka huu, jumla ya Vijiji
12,443, Vitongoji 64,616na Mitaa 3,741 vitahusika kwenye Uchaguzi.
Mheshimiwa
Spika, 12. Ili kufanikisha Uchaguzi huo, Serikali imekwishaandaa na kuchapisha
Vipeperushi, Fomu za Wagombea, Rejesta ya Wapiga Kura, karatasi za kuonyesha Vituo
vya Kupigia Kura, Mabango na Matangazo mengine kuhusu Elimu kwa Mpiga Kura. Tayari
vifaa hivyo vimepelekwa Mikoani na vingine vinaendelea kupelekwa. Aidha, Masanduku
ya Kupigia Kura yameshanunuliwa na tayari yameshasambazwa katika Mikoa yote Tanzania
Bara.
Mheshimiwa Spika, 13. Kwa vile siku zilizobakia kufikia tarehe ya
Kupiga Kura ni chache, natoa Wito kwa Wananchi ambao hawajajiandikisha katika Rejesta
ya Wapiga Kura wafanye hivyo bila kukosa. Aidha, Viongozi wa Vyama vya Siasa wawahimize
Wanachama wao na Wananchi kwa ujumla wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na hatimaye
wajitokeze siku ya Kupiga Kura. Aidha, Wasimamizi wa Uchaguzi wahakikishe vifaa vya
Uchaguzi vinafika kwenye maeneo yao kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, 14. Napenda
nitumie nafasi hii kutoa Rai kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa waendeshe kampeni kwa
amani na kuepuka maneno ya uchochezi, kubaguana kwa misingi ya ukabila, rangi, udini
ama hali ya mtu mambo ambayo yanaweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani. Aidha,
nawaomba Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wanachama wao, wakishapiga kura wasiendelee
kukaa katika Vituo vya Kupigia Kura, bali watawanyike na kusubiri muda wa matokeo.
HITIMISHO Mheshimiwa
Spika, 15. Leo nimeona nizungumzie masuala muhimu yanayochangia kusukuma Gurudumu
letu la Maendeleo. Kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru
wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika,
pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi
nzuri ya kuongoza vikao vya Bunge lako Tukufu. Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa
Wabunge kwa kazi nzuri na kwa michango mbalimbali wakati wa Mkutano huu.
Mheshimiwa
Spika, 16. Naomba pia nimshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja
na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi,
kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru
pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano
na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Niwashukuru Madereva kwa
kazi nzuri waliyofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge, Viongozi
mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.
Mheshimiwa
Spika, 17. Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu
ya kazi na katika majimbo yenu. Aidha, niwatakie mapumziko mema ya Sikukuu ya Christmas
na Mwaka Mpya wa 2015. Ninaamini kwamba, Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuvusha salama
sote kama tulivyo hadi kuuona Mwaka Mpya wa 2015. Baada ya kusema hayo, naomba sasa
kutoa Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 27 Januari, 2015 saa
3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 18kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma. Mheshimiwa
Spika, 18. Naomba kutoa Hoja.