2014-12-01 11:01:25

Vijana Wakimbizi msikatishwe tamaa na hali ngumu, hamko peke yenu..


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili katika mwelekeo wa kukamilisha ziara yake Istanbul Uturuki, alikutana na kundi la vijana wakimbizi kutoka Uturuki, Syria, Iraki na mataifa mengine ya Mashariki ya Kati na Afrika ambao wamepata hifadhi katika Kituo cha Shirika la Wasalesian cha Istanbul.

Mahali hapo, Papa aliwatazama vijana hao na kwa moyo wa kibaba na kuwaambia, uwepo wao hapo, unawakilisha idadi kubwa ya vijana wengi kama wao , waliolazimika kukimbia makazi yao na sasa wanaishi kama wakimbizi au wahamiaji katika maeneo mageni . Papa alihakikishia kwamba yupo pamoja nao katika mateso yao na alitumaini kukutana kwake nao na kwa neema ya Mungu , itakuwa ni faraja kwa hali ngumu, ambayo ni matokeo ya migogoro yenye ukatili na vita ambavyo daima huwa ni uovu na njia isizoweza kutoa ufumbuzi katika matatizo, badala yake huzua matatizo mapya .

Papa alionyesha kutambua hali ya wakimbizi kama wao , mara nyingi hukosa na wakati mwingine kwa muda mrefu mahitaji yao msingi, kama haki ya kuwa na makazi yanayostahili kuitwa “nyumbani” , huduma za afya , elimu na kazi. Na aliwaonea huruma kwamba, walilazimika kuacha mali zao , na hasa uhuru wao, familia na jamaa zao, aridhi na utamaduni wao . Na sasa wanalazimika kuishi hali duni, maisha ya wakimbizi, ambayo mara nyingi ni hayavumiliki.

Kwa kuziona hali hizo, Papa aliitumia nafasi hii , kuitaka dunia , ifanyike kila linaliwezekana, kuzuia kila sababu inayoweza kufanya watu wengine wakimbie nyumba zao na jamaa zao. Papa alieleza na kutoa wito kwa Jumuiya ya kimataifa kuwa na ushirikiano wa hali ya juu, katika juhudi za kupata ufumbuzi kwa migogoro inayozuka yenye kusababisha umwagaji wa damu , au kusababisha watu kukimbilia sehemu zingine zenye usalama zaidi kwa maisha yao.

Papa alihimiza usitishaji wa madhulumu na vita , ili wakimbizi waweze kurudi makwao. Na pia alihimiza watu wote kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya uwepo wa haki na amani, na bila kupoteza tumaini. Pia aliwataka wanasiasa , daima kukumbuka kwamba, watu wengi wanapenda amani , ingawa wakati mwingine hukosa nguvu za kupaza sauti zao, kudai haki hiyo.

Papa aligeukia mashirika ya misaada na kuyapongeza kwa huduma na msaada wake mzuri katika kusaidia wakimbizi. Na kwa namna ya kipekee alivitaja vikundi Katoliki ambavyo vimetoa kwa ukarimu msaada mkubwa kwa wahitaji tena bila ubaguzi. Na pia alitoa shukurani zake kwa Utawala wa Uturuki kwa jitihada kubwa katika kutoa msaada kwa watu waliokimbia makazi yao na hasa kutoka Syria na Iraki , na pia kwa ajili ya uwajibikaji a serikali unaotafuta kuhakikisha mahitaji ya wakimbizi yana patikana. Na hivyo Papa alionyesha tumaini lake kwamba , jumuiya ya kimataifa itakuwa nyuma ya kila juhudi , zinazo lenga kutoa wa msaada wa lazima kwa wakimbizi na wahamiaji.

Papa alikamilisha hotuba yake na mwaliko kwa vijana wakimbizi, kutokata tamaa, bali waendelee kujenga imani katika msaada wa Mungu, kwa siku za usoni, daima ni kuwa na tumaini la mabadiliko chanya, maisha mazuri , licha ya matatizo na vikwazo wanavyopambana navyo kwa wakati huu. Papa aliwahakikishia Kanisa Katoliki liko pamoja nao, kama inavyojionyesha kupitia kazi kubwa inayofanywa na kituo hiki kinacho wafadhili cha Wasalesiani. Aidha Kanisa Katoliki linajitahidi kutembea nao, kupitia huduma , mifumo na nafasi zingine mbalimbali kielimu na katika majiundo . Na daima wanapasa kukumbuka kwamba , Mungu hamsahau mja wake , hasa wanyonge na dhaifu wanaoteseka, daima wako katika mtima wa Baba wa Mbunguni.

Kwa upande wake, Papa alisema Pamoja na Kanisa zima la Ulimwengu, wanaendelea kutolea sala kwa Bwana , viongozi waviviwe na roho wa kukuza haki utulivu na amani kupitia njia mbalimbali za wazi na ufanisi. Kupitia mashirika yake ya kijamii na huduma, Kanisa daima linabaki upande wao na litaendelea kuwajali katika hali zote zinazowakabili duniani. Mungu awabariki nyote, Papa alikamilisha hotuba yake.








All the contents on this site are copyrighted ©.