2014-11-30 09:07:51

Watawa jitahidini kupyaisha maisha yenu kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji mpya!


Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya amezindua Mwaka wa Watawa Duniani, uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko utakaohitimishwa hapo tarehe 2 Februari 2016, kwa kuwataka watawa kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wao, ili kuweza kushiriki kikamilifu katika mchakato unaopania kupyaisha utume wa Uinjilishaji, huku wakiendelea kumtumikia Mungu na jirani zao.

Watawa wanatambua kwamba, mavuno ni mengi, lakini watendakazi katika shamba la Bwana ni wachache na kwamba, kwa wakati huu Mashirika mengi ya Kitawa na Kazi za Kitume yanakabiliwa na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha, hasa kutokana na kupungua kwa idadi ya miito ya maisha ya kitawa, kiasi cha kutia mashaka udumifu wa baadhi ya mashirika. Kardinali Njue amewataka watawa kuendelea kuwa na matumaini kwani Yesu mwenyewe atawakirimia yale wanayohitaji kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Mama Kanisa anapenda kutoa fursa hii kwa watawa kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wao na kuangalia ni kwa jinsi gani wamejitahidi kuwa waaminifu kwa Mungu na Kanisa hasa kwa kuzingatia Nadhiri zao, ili kuanza tena upya kwa kishindo na mwamko mkuu. Uinjilishaji wa kina unahitaji watu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika Mwaka wa Watawa Duniani litaandaa semina na kozi mbali mbali zitakazowasaidia watawa kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu.

Naye Askofu mkuu Charles D. Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya amewapongeza watawa kwa utume wao katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ameona na kushuhudia majitoleo ya watawa katika maisha na utume wa Kanisa hasa miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Katika utume wake kama Balozi wa Vatican nchini Kenya na Sudan ya Kusini ameonja sadaka kubwa inayotolewa na watawa kwa ajili ya Mungu na kuwashukuru na kwamba, umefika wakati wa kufanya tafakari ya kina, ili kuangalia jinsi ambavyo wanaweza kujisadaka zaidi, kwa kumwilisha karama ya Mashirika yao kati ya watu wanaowahudumia pamoja na kuendelea kuwa waaminifu kwa Mungu na kwa Kanisa.

Uzinduzi wa Mwaka wa Watawa Dunini huko Kenya, umehudhuriwa na viongozi mbali mbali kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya pamoja na watawa kutoka katika Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya ni "Watawa amkeni ili kuwaamsha walimwengu".







All the contents on this site are copyrighted ©.