Jumapili hii, ikiwa ni siku ya tatu na ya mwisho ya ziara ya Papa Francisco nchini
Uturuki ambako ametembelea miji ya Ankra na Istanbul, mapema asubuhi , ameifungua
kwa maadhimisho ya Misa binafsi, katika jengo la Uwakilishi Papa la jijini Istanbul.
Baada ya Misa, alikutana na Rabbi Mkuu wa Uturuki, Isak Haleva, kiongozi wa kiroho
wa Jumuiya ya Wayahudi wapatao 25, 000, wanaoishi Uturuki nchi ya Waislamu wengi.Wayahudi
wengi wanatajwa kuwa katika miji ya Istanbul na Izmir. Rabbi Haleva, pia aliwahi
kukutana na Papa mstaafu Benedikto XVI alipotembelea Uturuki Novemba 30, 2006.
Na
kisha Baba Mtakatifu Francisko, aliendelea na ratiba ya ziara yake kwa kutembelea
Kanisa la Mtakatifu George , ambayo ni Makao Makuu ya Upatriaki wa Kiekumeni wa
Constantinople, ambako alipokelewa na kukaribishwa Mwenyeji wake Patriaki Bartholomew
I, na kuongozana pamoja ndani ya Kanisa kwa ajili ya kuanza Maadhimisho Ibada kwa
mujibu wa Liturujia ya Maadhimisho ya Siku Kuu ya Mtakatifu Andrea Mtume.
Habari
inasema, ilikuwa ni jambo la kuvutia kuona Baba Mtakatifu, alipokutana na Patriaki
Bartholomeo I , aliinamisha kichwa chake kwa heshima kupokea baraka kutoka kwa Kiongozi
wa Kanisa la Kiothodox, na walikumbatia kwa heshima ikionyesha urafiki mkubwa na imara
kati yao. Pia inakumbukwa kwamba, mwaka jana, Patriaki Bartholomew I, alichukua hatua
ya kipekee ya kuja Roma kwa ajili ya uzinduzi wa Utawala wa Kitume wa Papa Francisko,
mara baada ya kuchaguliwa kuwa Papa, Mwezi Machi mwaka jana. Patriaki Bartholomew
I, akishiriki katika khafla hiyo, alitoa mwaliko kwa Papa aitembelee Uturuki wakati
wa kusherehekea sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Jumapili Novemba 30.
Na imevutia
jinsi Papa Francisco alivyozungukwa na Maaskofu waliovalia nguo nyeusi kutoka sehemu
mbalimbali za dunia ya Kanisa la Kigiriki la Kiotodosi. Papa amezungumzia ahadi
ya amani ya kweli ambayo Yesu alifanya na wanafunzi wake kwanza. Amesema, kama ilivyokuwa
kwa Petro na Andrea, kukutana kwao kama waandamizi wa Petro na Andrea, ni neema
na wajibu katika kutembea pamoja kama ndugu kwa matumaini ya Bwana Mfufuka. Na Patriaki,
ameeleza kuwa ziara hii ya Papa Francisko, inaendelea kuwa tukio la kihistoria lililo
jazwa na ishara za mazuri kwa siku za baadaye, kutembea pamoja katika njia ya kiekumeni.
Ameonyesha tumaini lake kwamba, ziara hii ya Papa Francisco ni hatua nyingine muhimu
katika barabara ya kuelekea kushinda mgawanyiko zamani, na kuwa na ubunifu mpya kwa
ajili ya uwepo wa ushirikiano mpya kati ya wale wote wanaoweka imani yao kwa Mungu.