Kuna maendeleo makubwa katika majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam!
Baba Mtakatifu Francisko, akiwa mjini Istanbul, Uturuki katika hija yake ya kiekumene,
Jumamosi 29 Novemba 2014 alipata nafasi ya kutembelea Msikiti mkuu wa Istanbul unaojulikana
kama Msikiti wa Bluu, hapo alipata nafasi ya kusali katika ukimya akiwa ameambatana
na Mufti mkuu. Alisikiliza kwa makini sehemu ya Korani Tukufu inayosimulia kutungwa
mimba kwa Yohane Mbatizaji kadiri ya mapokeo ya dini ya Kiislam.
Padre Federico
Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, hapa Baba Mtakatifu alibaki katika
ukimya, huku akiendelea kumwabudu Mwenyezi Mungu katika ukimya wa moyo wake. Wakati
wa mazungumzo yake na Mufti mkuu, Baba Mtakatifu Francisko amekazia umuhimu wa waamini
kusali na kumwabudu Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, changamoto ya kuendeleza
majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam, kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya waamini wa dini hizi mbili.
Baba Mtakatifu ametembelea pia Kanisa kuu la
Mtakatifu Yustini, moja ya maajabu makubwa ya kiufundi yanayoonesha hekima ya Mungu
katika maisha ya mwanadamu, lakini sasa Kanisa hili limegeuzwa kuwa ni Msikiti. Ameangalia
kwa umakini mkubwa mahali ambapo viongozi wa Kirumi kutoka Magharibi walikutana na
kuzungumza na baadaye akaandika maneno yanayoonesha hekima ya Mungu kwa lugha ya Kigriki.
Baba Mtakatifu amekutana na kusalimiana na baadhi ya waamini waliokuwa wamekusanyika
mbele ya Ubalozi wa Vatican nchini Uturuki. Amewashukuru na kuwapongeza wote kwa moyo
wa upendo na mshikamano wa dhati katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene
yanayojikita katika uhalisia wa maisha yao.