2014-11-30 09:28:01

Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia linaadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya uhai wake!


Askofu mkuu Berhaneyesus D. Souraphiel wa Jimbo kuu la Addis Ababa, Ethiopia, hivi karibuni alizindua maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia na kilele cha maadhimisho haya ni hapo tarehe 26 Julai 2015. Maadhimisho yanaendelea kutimua vumbi katika Majimbo mbali mbali nchini humo.

Kuanzia tarehe 3 hadi tarehe 5 Desemba 2014 kunafanyika Kongamano la Kitaifa, litakalochambua kwa kina na mapana maisha na utume wa Kanisa nchini Ethiopia katika kipindi cha miaka 50 iliyopita kwa kuangalia changamoto zilizopo katika kuifunda mihimili ya Uinjilishaji; mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki nchini Ethiopia pamoja na kuonesha mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika kipindi cha miaka 50 ya uhai wake, hasa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia katika kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya uhai wake, linatarajiwa kuchapisha kitabu kitakachoweka kumbu kumbu ya matukio yote haya kwa ajili ya kuwasaidia waamini kutambua mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya watu nchini Ethiopia. Kanisa limefanikiwa kupata viongozi mahalia, kwani Baraza lilipoanzishwa lilikuwa na Maaskofu watatu, lakini leo hii kuna Maaskofu kumi na watatu na idadi ya majimbo imeongezeka maradufu ili kuboresha huduma za maisha ya kiroho kwa watu. Huduma zinazotolewa na Mama Kanisa nchini Ethiopia ni kwa wananchi wote pasipo na ubaguzi.







All the contents on this site are copyrighted ©.