2014-11-28 14:19:53

Waandishi wa habari 65 wako kwenye msafara wa Papa Francisko nchini Uturuki!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kiekumene nchini Uturuki, Ijumaa tarehe 28 Novemba 2014 amepata nafasi ya kuzungumza kidogo na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwa kuwataka kutekeleza dhamana yao kikamilifu ili kuhabarisha ulimwengu shughuli mbali mbali za kidini na kijamii zinazotekelezwa na Makanisa kwa ajili ya mafao na maendeleo ya wengi. Uturuki kwa wakati huu inafanya kazi kubwa ya kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji ambao wanatafuta hifadhi ya maisha ugenini kutokana na dhuluma na nyanyaso za kidini zinazoendelea huko Mashariki ya Kati.

Baba Mtakatifu anawashukuru waandishi wa habari kwa huduma hii makini kwa ajili ya watu sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, ataweza kuzungumza nao kwa kina na mapana, mara baada ya kuhitimisha hija yake ya kiekumene huko Uturuki ambako anapania kujenga na kudumisha misingi ya majadiliano ya kiekumene na ugudu kati ya watu, ili waweze kuheshimiana na kusaidiana kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mungu.

Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari, amemhakikishia Baba Mtakatifu sala kutoka kwa Waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake, ili hija hii ya kiekumene iweze kudumisha mahusiano ya kiekumene sanjari na kukuza majadiliano ya kidini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Msafara wa Baba Mtakatifu nchini Uturuki unasindikizwa na waandishi wa habari 65 kutoka katika tasnia ya habari ndani na nje ya Italia; tayari kuwahabarisha walimwengu yale yanayotendeka huko Uturuki. Waandishi wa habari wamemhakikishia Baba Mtakatifu kwamba, wanapenda kumsaidia kufikisha ujumbe anaokusudia kwa wananchi walioko ndani na nje ya Uturuki kwa njia ya vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya kijamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.