Waamini walei wanatumwa na Mama Kanisa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda
wa imani tendaji!
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwenye Tamko lao kuhusu Waamini Walei, wanasema,
walei wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwani kwa
njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki huduma za Kristo za kikuhani, kinabii na
kifalme.
Ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za
Kanisa ni jambo linalohimizwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, sanjari
na kukazia maisha ya kiroho, ili kuwawezesha waamini walei kuyatakatifuza malimwengu,
wakifanya yote kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Waamini walei wajitoe bila ya
kujibakiza katika mchakato wa kuinjilisha na kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya
ushuhuda amini wa maisha yao, huku wakipenyeza roho ya Kikristo katika medani mbali
mbali za maisha.
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanataka waamini
walei kushiriki kikamilifu katika kuanzisha na kuendeleza vyama vya kitume katika
ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa mahalia pamoja na kuzingatia mahitaji
ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zipewe
kipaumbele cha kwanza; vijana wasaidiwe kukua na kukomaa katika kanuni na misingi
bora ya maadili, ili wawe kweli ni "majembe" ya Uinjilishaji miongoni mwa vijana wenzao.
Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, katika Warsha ya
Idara ya Waamini Walei, AMECEA, inasema kwamba, majiundo kwa waamini walei ni kati
ya mambo ambayo AMECEA inataka kuyapatia kipaumbele cha kwanza katika shughuli na
mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Haya yamebainishwa na Askofu Philip Anyoli,
alipokuwa anazungumza na wajumbe waliokuwa wanachambua Utume wa Waamini Walei, mkutano
ambao umefanyika Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Wajumbe wamehamasishwa kuibua
mbinu mkakati utakaoimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuweza
kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Familia inaendelea kuwa ni
madhabahu ya Injili ya Uhai; mahali ambapo zawadi ya maisha inapokelewa, inatunzwa
na kuendelezwa, hadi kufikia ukamilifu wake. Maisha ya binadamu yanarithishwa kwa
njia ya familia, pasi na familia, ulimwengu utatumbukia katika ombwe zito, kwani familia
ni msingi wa jamii.
Waamini walei wanakumbushwa kwamba, wao ni sehemu ya majembe
yanayotegemewa na Mama Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, unaozingatia mahitaji
ya mtu mzima: kiroho na kimwili, changamoto ya kuwa kweli ni chumvi na mwanga wa mataifa,
kwa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika medani mbali mbali za maisha,
ili kuyatakatifuza malimwengu kama anavyokazia Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI
katika Waraka wake wa Kichungaji, Dhamana ya Afrika. Ili kutekeleza dhamana hii, waamini
walei hawana budi kulifahamu Neno la Mungu, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki pamoja
na Mafundisho Jamii ya Kanisa, nyenzo muhimu katika kuyatakatifuza malimwengu.
Askofu
Telesphori Mkude, Mwenyekiti wa Idara ya Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
amewaambia wajumbe wa Warsha hii kwamba, familia katika ulimwengu mambo leo inakabiliana
na matatizo, changamoto na fursa nyingi ambazo Mama Kanisa anapaswa kuziangalia kwa:
huruma, uelewa na mapendo, ili kuganga na kuponya madonda yanayoibuliwa ndani ya Familia
kwa kutumia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Matatizo kama uchumba sugu, ndoa
za wake wengi; ndoa za watu wajinsia moja ni changamoto kubwa katika Sakramenti ya
ndoa na tunu msingi za maisha ya kifamilia.
Askofu Mkude anasema, maadhimisho
ya Sinodi za Maaskofu kwa ajili ya Familia yanayofanyika katika awamu kuu mbili ni
jambo ambalo limekuja kwa wakati muafaka, ili kulipatia Kanisa nafasi ya kuangalia
changamoto za kichungaji katika maisha ya ndoa na familia, ili kuweza kuwa na mwongozo
kamili.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Askofu Desiderius Rwoma, Mwenyekiti
wa Idara ya Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, iliyosomwa kwa niaba yake
na Askofu msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki la Bukoba, ameelezea kwa kina
na mapana, matatizo yanayowakumba watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, kiasi
cha kukosa fursa za elimu, afya, malezi na majiundo makini na matokeo yake wanajikuta
wakitumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo pamoja na kufanyishwa
kazi za suluba, mambo ambao yanahatarisha makuzi, ustawi na maendeleo ya watoto hao.
Askofu
Rwoma anasema kwamba, chanzo kikubwa cha ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi ni umaskini, kumong'onyoka kwa: maadili sanjari na misingi bora ya ndoa
na familia; sera na mikakati duni ya kijamii na kiuchumi. Umefika wakati kwa Jamii
Barani Afrika kusimama kidete kupinga kwa nguvu zote: utumwa wa aina zote wanaofanyiwa
watoto, ili kulinda na kudumisha haki zao msingi. Watoto wasifanyishwe kazi za suluba,
wala kuhusishwa katika utumwa mamboleo au kupelekwa mstari wa mbele pamoja na kunyanyaswa
utu na heshima yao.
Askofu Rwoma amewapongeza Wanawake Wakatoliki wanaoshiriki
kikamilifu katika kuyategemeza Makanisa mahalia kwa kuziwezesha Seminari na Nyumba
za Malezi kupata mahitaji yao msingi pamoja na kupambana na mila na desturi ambazo
zimepitwa na wakati kwa mfano ukeketaji wa wanawake. Kanisa linawashukuru Wanaume
Wakatoliki wanaoendelea kulijenga Kanisa kwa juhudi na maarifa pamoja na kutumia vipaji
vyao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.
Warsha hii imehudhuriwa
na wajumbe 60 kutoka katika Nchi za AMECEA na ilikuwa inaongozwa na kauli mbiu "Ndoa
na Maisha ya Familia, Kanisa na Jamii kwa siku za usoni. Kwa mara ya kwanza, Warsha
hii imehudhuriwa na wajumbe wengi zaidi kutoka katika Nchi za AMECEA, ikilinganishwa
na miaka mingine iliyopita. wajumbe kutoka Djibouti, Somalia, Zimbabwe na Mauritius
wameshiriki kwa ukamilifu, matendo makuu ya Mungu.
Itakumbukwa kwamba, tangu
Mwaka 1975, Baraza la Waamini Walei, katika Nchi za AMECEA lilianzishwa, lakini limeendelea
kusinzia kwa miaka yote hii bila hata kutekeleza utume na dhamana yake katika nchi
za AMECEA. Mwaka huu, wajumbe wanasema, watajadili hadi kieleweke!
Na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.