2014-11-28 15:33:48

Uturuki ina jukumu kubwa, mfano wa amani na msaada mkubwa katika makutano ya staraabu


Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Uturuki majira ya mchana, alipokelewa na Rais wa Jamhuri ya Uturuki, katika khafla iliyopambwa na nyimbo za kitaifa za nchi mbili Vatican na Uturuki na gwaride la heshima la Maaskari, ambako pia ujumbe wa wawakilishi kutoka pande zote mbili ulitambulishwa.

Kisha Mheshimiwa Rais Recep Tayyip Erdogan, alimchukua mgeni wake Papa ndani ya Ikulu ambapo walifanya mazungumzo katika hali ya faragha na baadaye kuuangana na wengine na kuhutubia. Ziara ya Papa Francisco inaendeleza mema yaliyofanywa na watangulizi wake , Mwenye Heri Papa Paulo VI, Mtakatifu Yohane Paul II na Papa Mstaafu Benedict XVI, kuendeleza mazungumzo kwa heshima na taadhima kati ya utawala wa Kanisa Katoliki na viongozi wa Uturuki, katika mtazamo wa Kanisa, Kanisa lisilo jifungia ndani lakini kutoka nje na kukutana na watu kama ilivyoazimwa katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Papa Francisco, akikutana na viongozi wa ngazi ya juu katika Utawala wa Uturuki, hotuba yake zaidi ililenga katika udumishaji wa historia wa taifa hili, ambako bado kuna utajiri mkubwa wa mabaki ya ustaarabu wa kale, na kama daraja asilia kati ya mabara mawili Asia na Ulaya ,na kati ya tamaduni mbili tofauti , nchi ya Mtakatifu Paul, ambako alianzisha jumuiya mbalimbali ya Kikristo; nchi ya Mabaraza saba ya kwanza ya Kanisa. Na pia karibu Efeso, mahali panapofahamika uwepo wa nyumba na Bikira Mariam, mahali ambapo mama wa Yesu aliishi kwa miaka michache, ambako mahujaji toka sehemu mbalimbali za dunia hupatembelea si tu Wakristo, lakini pia Waislamu.

Papa Francisco amesisitiza viongozi wa serikali, haja ya kuongeza mazungumzo kwa ajili ya kuongeza maarifa na maadili na utambuzi mambo mengi yanayo uganisha jamii kwa nyakati hizi, na wakati huohuo kuruhusu kila mmoja kukiishi anachokiamini na fikira tofauti, kama sehemu ya mwendelezo wa jitihada za kujenga amani imara, kwa misingi kuheshimu haki msingi na wajibu, na hadhi ya binadamu. Ili hatimaye, Waamini wa dini kuu tatu Waislamu, Wayahudi na Wakristo, kwa mujibu wa sheria, waweze kwa ufanisi kutekeleza na kufurahia haki sawa na kuzingatia majukumu sawa, Uhuru wa dini na uhuru wa kujieleza, kuwa jambo la uhakika kwa wote, n akama chombo cha amani.

Papa ameonyesha masikitiko yake kwamba, Mashariki ya Kati kwa muda mrefu imekuwa ukumbi wa migawanyiko ya kivita, ambavyo huanzishwa na kukuzwa n ubabe wa kulipiza visasi, mmoja kwa mwingine, kama vile, ghasia na vita ni jibu pekee la kunyamazisha hali hiyo. Lakini imekwisha thibitishwa kwamba vita haiwezi kunyamazisha vita. Jibu kuu katika kunyamazisha vita ni uaminifu katika maamuzi yanayo fikiwa katika njia zote za mazungumzo, yanayolenga kufikia lengo halisi la uwepo wa amani na maendeleo endelevu.

Aliongeza kuwa, pia mchango muhimu katika kufanikisha amani , unaweza patikana kupitia majadiliano kati ya dini, na utamaduni wa mazungumzo, silaha inayofaa kuondoa aina yoyote ya ubabe na ugaidi, ambayo hudhalilisha hadhi ya watu wote kwa kutumia jina la dini. Ni kupinga ushabiki huu wa kupindukia, badala yake waumini wote kuwa na umoja lakini katika utofauti wao na kushikamana kwa nguzo heshima kwa maisha ya binadamu, uhuru wa kuabudu na uhuru wa kuishi kulingana na maadili ya kidini, na juhudi za kuhakikisha kwamba, binadamu wote wana haki ya kuishi maisha ya heshima na huduma katika mazingira yao asili.

Papa ametaja kuwa nii ni hoja na changamoto ya sasa Mashariki ya Kati , kama jambo la kidharura, kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika wimbi la machafuko ya kivita. Wanahitaji kuzima wimbi hili kwa kuingia katika mchakato wa majadiliano ya amani, kuikataa njia ya vita na vurugu. Badala yake ni kuanzisha harakati za mazungumzo ya haki na usawa.

Papa Francisko ameeleza kwa kurejea mgogoro mkubwa wa vita Syria na Iraq, na hasa, vurugu kigaidi, ukiukaji wa sheria ya msingi dhidi ya binadamu, kama inavyoshuhudiwa dhidi ya wafungwa na makundi yote ya kikabila, mateso makali dhidi ya vikundi vya watu wachache, hasa - lakini si tu -, Wakristo na Yazidis, lakini mamia ya maelfu ya watu waliolazimika kukimbia makazi yao na nchi yao ili kuokoa maisha yao na kubaki na imani yao.

Papa alikamilisha hotuba yake na shukurani kwa taifa la Uturuki kwa ukarimu wake wa kupokea idadi kubwa ya wakimbizi. Na akaihimiza Jumuiya ya kimataifa kwamba, ina wajibu wa kimaadili kusaidia katika Uturuki kuhudumia wakimbizi hao. Na kwamba haiwezekani kuendelea kukalia kimya kilichosababisha majanga haya. Ni lazima kutafuta njia za kusitisha uchokozi na madhulumu, lakini daima kwa kufuata sheria ya kimataifa.

Na haiwezekani kuendelea kutegemea kukabiliana na wachokozi kwa njia na majibu ya kijeshi. Lazima ni muhimu na lazima kuelekeza nguvu na rasilimali si katika kuwa na wingi wa silaha, lakini katika mapambano dhidi ya njaa na magonjwa, kwa ajili ya maendeleo endelevu na ulinzi wa viumbe, na dharura nyingine nyingi zenye kusababisha umaskini na watu kutengwa.

Uturuki, kwa historia yake, sababu ya nafasi yake ya kijiografia na kwa umuhimu wake katika kanda ya Mashariki ya Kati , ina jukumu kubwa, la kuwa mfano maalum, na msaada mkubwa katika kuwezesha mikutano ya ustaarabu na kutambua njia halisi za kuleta amani na maendeleo halisi, kwa ajili ya ustawi wa watu wa Mashariki ya kati. .









All the contents on this site are copyrighted ©.