Hija ya Papa Francisko nchini Uturuki, lengo ni kuimarisha: majadiliano na udugu
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko
nchini Uturuki kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Novemba, 2014 ni kutaka kuimarisha
na kudumisha majadiliano ya Kiekumene kati ya Wakristo; udugu kati ya watu pamoja
na kuendeleza mchakato wa haki na amani huko Mashariki ya Kati.
Baba Mtakatifu
katika hija hii ya kitume, wataadhimisha kwa pamoja Siku kuu ya Mtakatifu Andrea na
kutia sahihi tamko la pamoja kuhusu majadiliano ya kiekumene, mwendelezo wa tamko
lililotiwa sahihi wakati Baba Mtakatifu Francisko alipofanya hija ya kichungaji katika
Nchi Takatifu, kunako mwaka 2014. Lengo ni kuimarisha misingi ya upendo, udugu na
mshikamano, pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea: haki na amani sanjari na
uhuru wa kuabudu huko Mashariki ya Kati, ambako kuna idadi kubwa ya Wakristo wanaoendelea
kuteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Ili
amani ya kweli iweze kupatikana huko Mashariki ya Kati kuna haja kwa pande zote zinazohusika
kuweka silaha chini ya kuanza kujikita katika majadiliano yanayojikita katika ukweli,
uwazi na upatanisho; lakini ukweli wa mambo mchakato wa amani unaendelea kupambana
na kinzani nyingi kiasi hata cha kuwakatisha wananchi tamaa ya kupata amani ya kweli.
Kardinali
Parolin anasea, dhamana na utume wa Kanisa ni kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa
watu wanaoteseka na kunyanyasika; watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia
usalama wa maisha yao, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuchukua hatua zinazofaa ili
kuwalinda watu hao. Kanisa kwa kutumia Mashirika yake ya misaada linaendelea kuwahudumia
wakimbizi na wote wanaohitaji huduma bila ya ubaguzi. Kipindi cha baridi, hali itakuwa
ni mbaya sana, kumbe, Kanisa linaendelea kukazia umuhimu wa watu kurejea tena kwenye
makazi yao.
Kanisa Katoliki nchini Uturuki ni kundi dogo ambalo nalo limepitia
katika majaribu makubwa, lakini bado lipo na linaendelea kutoa ushuhuda wa utume wake
kwa njia ya majadiliano ya kidini na Waamini wa dini ya Kiislam.