Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linasema kwamba, utoaji mimba si sehemu ya haki
msingi za binadamu bali ni kwenda kinyume cha Injili ya uhai, utu na heshima ya binadamu,
ni mwelekeo wa jamii kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo kwa kisingizio cha uhuru
wa wanawake kuamua wanavyotaka kuhusiana na miili yao! Maaskofu wanasema, ni vigumu
kuonesha kwamba, utoaji mimba ni sehemu ya haki msingi za binadamu wakati unapelekea
mauaji ya kiumbe kisichokuwa na hatia.
Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa
linasema kwamba, harakati za kutaka kukuza na kudumisha uhuru na usawa kati ya wanawake
na wanaume ni mambo mazuri katika jamii, lakini usawa unaotoa haki ya mtu kushiriki
katika mauaji ya watoto wasiokuwa na hatia hapa ni kwenda kinyume kabisa cha haki
msingi za binadamu pamoja na kuwasababishia mateso na mahangaiko makuba wanawake wanaoshiriki
katika zoezi la utoaji mimba. Kuna kundi kubwa la wanawake linaloendelea kuteseka
kisaokolojia na kwa vile waliwahi kushiriki katika zoezi la utoaji mimba, lakini ni
mateso na mahangaiko ambayo hayazungumziwi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa
linasema, uhuru ni muhimu sana katika kukuza na kuendeleza mahusiano kati ya mwanaume
na mwanamke, wanaotambua dhamana na wajibu wao unaowashirikisha katika kazi ya uumbaji.
Kumbe, huu ni uhuru unaowajibisha na kuhamasisha majadiliano ya kina. Kumbe, kuna
haja kwa jamii kuangalia kwa makini kwamba, mimba isionekane kuwa ni jambo ambalo
halitakiwi na inaweza kuondolewa wakati wowote ule, kwani mtoto aliyeko tumbani mwa
mama yake ana haki ya kuzaliwa, kukua na kukomaa kadiri ya mapenzi ya Mungu.