Tuzo ya Joseph Ratzinger yatolewa kwa wasomi waliobobea katika Neno la Mungu!
Kardinali Gerhard Ludwig Mùller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu
ya Kanisa, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 22 Novemba 2014
alitoa tuzo ya nne ya "Joseph Ratzinger" kwa wasomi waliobobea katika tafiti za kitaalimungu,
kama njia ya kuenzi mchango mkubwa uliotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
XVI katika taalimungu.
Kwa mara ya kwanza, tuzo hii imetolewa kwa Professa
Anne Marie Pelletier, Mwanamke, anayefundisha Maandiko Matakatifu katika Chuo Kikuu
cha Biblia mjini Paris, Ufaransa, Tuzo hii pia amepewa Padre Waldermar Chrostowski,
mtaalamu wa Maandiko Matakatifu anayejibidisha katika kukoleza majadiliano kati ya
Wakristo na Wayahudi.
Kardinali Mùller katika hotuba yake amekazia umuhimu
kwa Wakleri, Majaalim, Walimu wa dini, wadau mbali mbali katika shughuli za kichungaji
na Wakristo katika ujumla wao, kuhakikisha kwamba, wanajibidisha kujisomea na kufanya
tafiti kuhusu mchango wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika taalimungu.
Josefu
Ratzinger ni kiongozi kama alivyowahi kusema Papa Francisko aliyefanya tafiti zake
za Kitaalimungu kwa kupiga magoti, yaani kazi zake ni matunda ya tafakari ya kina
inayosimikwa katika sala. Imani ina nafasi ya pekee katika hija ya maisha ya waamini
kwani inawaangazia mwanga katika akili zao ili kutambua mapenzi ya Mungu.
Ikumbukwe
kwamba, taalimungu si tu elimu inayomzungumzia Mwenyezi Mungu, bali ni matunda ya
ya tafiti makini zilizofanywa na akili mintarafu Neno la Mungu linalozungumza kuhusu
Mungu mwenyewe, kwani huu ni mchakato wa majadiliano ya ndani yanayomhusisha binadamu.
Naye
Monsinyo Giuseppe Scotti, Rais wa Mfuko wa Joseph Ratzinger, katika hotuba yake ya
ufunguzi amewatambulisha washindi wa tuzo hii kuwa ni watu ambao wamefanya hija ya
maisha na tafiti zao huku wakiwa wamekamia kusonga mbele kwa imani na matumaini bila
ya kuyumbishwa.
Kwa upande wake, Kardinali Camillo Ruini, Rais wa Kamati ya
Kisayansi ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, amefafanua wasifu na mchango wa Mama Anne-
Marie Pelletier na Monsinyo Waldermar Chrostowski. NI watafiti wanaoesha mchango mkubwa
wa Kanisa Katoliki nchini Ufaransa katika masuala ya kitaalimungu na uhai katika maisha
ya kitamaduni, kama kielelezo makini cha ushuhuda wa Kikristo ndani ya Jamii.
Monsinyo
Chrostowski kutoka Poland ni Mhariri mkuu wa Jarida la Kitaalimungu nchini mwake.
Ni msomi mwenye ari na moyo mkuu, anayefahamu kwa kina na mapana Maandiko Matakatifu;
utajiri anaowashirikisha wengine kwa njia ya kufundisha, tafiti za maisha ya kiroho
pamoja na kuwaongoza mahujaji katika maisha yao ya kiroho. Ni kiongozi anayejipambanua
kwa kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi.
Ni
mtaalam anayefahamu kuunganisha kanuni za kisayansi na usongo wa Neno la Mungu, kwa
ajili ya huduma kwa Kanisa katika mchakato wa maendeleo ya majadiliano ya kidini,
changamoto endelevu iliyotoewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, dhana
inayovaliwa njuga kwa wakati huu na Baba Mtakatifu Francisko.