2014-11-23 14:43:16

Mkicheza na masomo, mtakiona kilichomnyoa Kanga manyoya!


Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu vya mkoa wa Dodoma watumie fursa waliyonayo kuisaidia nchi ya Tanzania isonge mbele na kufikia uchumi wa juu zaidi. Alitoa nasaha hizo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wanavyuo hao kwenye ukumbi wa Chimwaga, Dodoma wakati wa mkesha wa kusifu na kuabudu (Dodoma Campus Night) ulioandaliwa maalum kwa ajili ya kuwajenga kimaadili wanafunzi wa vyuo vya mkoa huo.

Dk. Nchimbi ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kabla ya kuhamishiwa Njombe, aliwaasa wanafunzi hao waache kuendekeza matumizi ya simu za mkononi kwa kutumiana ujumbe ambazo zinawatoa kwenye umakini wa masomo yao. “Inasikitisha kuona mwanafunzi akiingia mwaka wa kwanza anakuwa mwema, lakini baada ya muda anarudi nyuma kimaendeleo… kisa meseji anazotumiwa”.

“Muwe makini na masomo yenu. Angalieni mavazi yenu, angalieni mienendo yenu, jichungeni msiyumbishwe na tabia za makundi lakini kikubwa zaidi ni kutambua nafasi mlizonazo na kusimama imara ili kuisadia nchi hii isonge mbele na kufikia uchumi wa juu zaidi,” alisema.

Mapema, akimkaribisha kuzungumza na wanafunzi hao, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la TAG-ICC Dodoma, Dk. Gerald Ole Nguyaine aliwaambia wanavyuo kwamba wanapaswa kuiheshimu nafasi hiyo ya pekee ambayo Mungu amewapa. “Hebu jiulize ni wanafunzi wangapi ambao wamebaki huko nje na wanatamani kuingia Chuo Kikuu… ni lazima muwe na dira ili kuitendea haki nafasi mliyoipata. Na kama unataka kuwa mtu ambaye Mungu alikusudia uwe, ni lazima ujisalimishe kwake,”alisema.

Akitoa mafundisho kwa wanavyuo hao, Mchungaji Casey Kalaso wa Kanisa la Utume wa Kristo kutoka Kabwe, Zambia aliwataka wanavyuo hao watambue kuwa mafanikio yanakuja pale mtu anapofanya maandalizi na kutumia vizuri fursa aliyonayo. “Changamoto kuwa inayotukabili hivi sasa ni kwa mwanadamu kutojua majira aliyomo… watu wengi hatujui nini tunapaswa kufanya na kwa wakati gani. Usipokuwa mwangalifu utalia baadaye wakati ulichezea fursa uliyoipata sasa,” alisema.

Akitumia mfano wa Samson na Delila kutoka kitabu cha Waamuzi (sura ya 13), aliwataka waithamini nafasi waliyonayo kwani ikipotea ni nadra kuipata tena na kuitumia vizuri. “Usiangalie mambo ya nyuma, angalia nafasi ya sasa unayopewa na Mungu na uifanyie kazi. Jihadhari na watu wanaokuja maisha mwako, wako wanaokuja kukuongezea thamani lakini wengine wanakuja ili kukufanya uwe dhaifu zaidi,” aliwaonya.

Naye Mchungaji Mathew Sasali wa Kanisa la TAG Mbeya aliwataka wanavyuo hao wajitambue nafsi zao na kubaini ni picha gani ambazo zimechorwa maishani mwao kama kweli wanataka kusonga mbele maishani mwao. “Kuna watu waliambiwa hutafaulu kwa sababu katika ukoo wenu hakuna msomi, au fulani hutaolewa kwa sababu katika familia yenu hakuna aliyewahi kuolewa. Hizo zote ni picha zinazochorwa kwenye maisha ya watu na kuwazuia kufikia malengo wanayotamani kuyapata maishani mwao,” alisema.

“Kama hujagundua kuwa kuna picha imechorwa maishani mwako ni lazima tu itakutesa. Hiyo picha inatabiri ni vita ya aina gani unapigana nayo. Na usipoifuta hiyo picha, huwezi kutoka kwenye maisha uliyonayo… iwe ni ulevi, uzinzi, uvivu, na kadhalika,” alisema.

Alisema njia pekee ni kuibadilisha na kupambana na picha iliyowekwa mbele ya maisha yao. “Picha iliyo mbele yako siyo ile ambayo Mungu ameileta mbele yako. Taifa la Israel lisingeweza kwenda mbele kama picha nyingine isingechorwa mbele yao ambayo ilibadilishwa na Yoshua na Kaleb,” alisisitiza.

Ninawasihi tuchane picha zilizoletwa mbele yetu, iwe na ndugu, marafiki, wanaukoo au wachawi. Tuchukue hatua na kuikataa picha iliyo mbele yetu ambayo iko nje ya mpango wa Mungu. Fahamu zetu zikifunguka na kuiona picha ya Mungu, ndipo tutaanza kuchanua na kufanikiwa,” alisema.

Katika Campus Night hiyo ambayo ilihudhuriwa na wanavyuo zaidi ya 5,000, yalifanyika pia maombi kwa ajili ya vijana wote wa Tanzania, uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Uchaguzi Mkuu wa 2015 pamoja na mchakato wa Katiba Inayopendekezwa. Wanavyuo hao wa dini mbalimbali wanatoka vyuo vikuu vya Dodoma (UDOM), St. John’s, Vyuo vya Mipango, Madini, Mirembe, Hombolo, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na vyuo vya ualimu vya Mitumba na Capital.








All the contents on this site are copyrighted ©.