Jengeni na kudumisha moyo wa ushirikiano na maridhiano kwa jili ya mafao ya wengi!
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya maadhimisho ya Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme
wa Ulimwengu sanjari na kuwatangaza watakatifu wapya sita, aliwashukuru wawakilishi
kutoka katika nchi wanamotoka watakatifu hawa kwa kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu,
lakini zaidi amewataka wananchi wa Italia kujenga na kudumisha moyo wa ushirikiano
na mapatano kwa ajili ya mafao ya wengi, huku wakionesha matumaini kwa kesho iliyo
bora pamoja na kutumainia uwepo wa Mungu ambaye daima amekuwa karibu nao na kamwe
hawezi kuwaacha katika nyakati ngumu za maisha.
Kwa watakatifu wawili wanaotoka
India, nchi ambayo ni chemchemi kubwa ya miito ya kipadre na kitawa, Mwenyezi Mungu
asaidie kuleta mwamko mpya wa Kimissionari kwa Kanisa nchini India, kwa kujikita katika
maridhiano na upatanisho, ili Wakristo nchini India waweze kusonga mbele katika hija
ya mshikamano na maisha ya kidugu. Familia yote ya Mungu imewekwa chini ya ulinzi
na usimamizi wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, Malkia wa Watakatifu na mfano
wa Wakristo.