Igeni: imani, mapendo na matumaini kutoka kwa Watakatifu wapya!
Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu ni mwaliko kwa waamini kumwangalia Yesu
ambaye ni Mfalme wa kweli na uzima; utakatifu na neema; haki, mapendo na amani. Waamini
wanaoneshwa jinsi ambavyo Yesu mwenyewe amemwilisha ufalme huu katika historia na
maisha ya mwanadamu kwa kujionesha kuwa ni mchungaji mwema anayepanda na kuwaongoza
kondoo wake kwenye malisho ya majani mabichi, anawatafuta wale alipotoea na kuwaganga
wagonjwa na wale waliopondeka moyo! Yesu ni kielelezo kwa viongozi wa Kanisa ambao
wanahamasishwa kuwa ni wachungaji wema wanaojitofautisha na wevi na wanyang'anyi!
Hii
ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya
Misa katika maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme sanjari na kuwatangaza Wenyeheri
sita kuwa ni watakatifu. Yesu kwa njia ya ufufuko wake, ameshinda kifo na mauti na
hivyo anatawala milele huku akiwaonjesha watu upendo na wokovu.
Injili inaonesha
jinsi ambavyo Yesu atakavyotoa hukumu ya mwisho, kwa kuwashirikisha wateule wake Ufalme
wa Mungu ulioandaliwa kwa ajili yao tangu milele, kwani walionesha upendo na mshikamano
kwa maskini pamoja na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Wokovu unapata
chimbuko lake pale mwamini anapojitahidi kuiga matendo ya huruma yanayoonesha utimilifu
wa Ufalme wa Mungu, kwani matendo haya ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwa binadamu.
Watu watahukumiwa kwa jinsi ambavyo wamemwilisha upendo huu kwa jirani zao, kwa njia
ya ukarimu na mshikamano, kiini cha Injili.
Watakatifu wapya ni kielelezo makini
cha watu waliojisadaka kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani, kila mtu akajitahidi
kuchangia kadiri ya uwezo wake katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Ni watakatifu waliojipambanua
kwa huduma makini kwa maskini, wagonjwa, wazee na mahujaji pamoja na kutoa katekesi;
wakaonesha mkazo zaidi kwa wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, hawa
ndio waliobarikiwa na Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya kuwatangaza
Wenyeheri kuwa watakatifu, Kanisa limekiri Fumbo la Ufalme wa Mungu kwa kumheshimu
Kristo Mfalme na Mchungaji mwema, anayeonesha upendo wa hali ya juu kwa Kondoo wake.
Watakati wapya wawasaidie na kuwaombea waamini kukua katika furaha ya kutembea katika
njia ya Injili na kuimwilisha, ili iweze kuwa ni dira katika maisha. Waamini wajifunze
kutoka kwa watakatifu wapya: imani, mapendo na matumaini yasiyofifia kamwe bila kumezwa
na malimwengu.
Watakatifu waliotangazwa na Baba Mtakatifu wakati wa Maadhimisho
ya Sherehe ya Kristo Mfalme, ambao historia ya maisha na utume wao imesomwa na Kardinali
Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri
na watakatifu ni hawa wafuatao:
Giovanni Antonio Farina Kuriakose Elias
Chavara wa Familia Takatifu Ludovico Casoria Nicola de Longobardi Eufrasia
Eluvathingal wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Amato Ronconi