Katika maadhimisho ya Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu, Jumapili asubuhi,
tarehe 23 Novemba 2014, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa
Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pamoja na kuwatangaza
Wenyeheri sita kuwa Watakatifu.
Hawa ni Mwenyeheri Giovanni Antonio Farina,
Askofu; Kuriakose Elias CHavara wa Familia Takatifu, Padre; Ludovico wa Casoria, Padre;
Nicola wa Longobardi, Mtawa, Aufrasia Eluvathingal wa Moyo Mtakatifu wa Yesu pamoja
na Mwenyeheri Amato Ronconi, Mtawa, Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Francisko.
Kanisa
linasherehekea Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa mbingu na dunia, enzi na utawala
vyote ni vyake, changamoto na mwaliko kwa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema
kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa
katika: ukweli na uzima; Utakatifu na Neema; Haki, Mapendo na Amani.