Pyaisheni karama zenu; wapokeeni na kuwasindika vijana ili kujenga umoja!
Kongamano la tatu la Vyama vya kitume na Jumuiya mpya, lililokuwa linaongozwa na kauli
mbiu "Furaha ya Injili: ni furaha ya kimissionari" lililoandaliwa na Baraza la Kipapa
la Walei, limejadili kwa kina na mapana changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko
ya kukuza na kukoleza ari na moyo wa kimissionari ili kuwashirikisha wengine Injili
ya Furaha, kwa kutambua kwamba, wanaitwa kutoka katika ubinafsi wao, ili kuanza hija
ya maisha ya kiroho kwa ajili ya kuwashirikisha wengine Injili ya Furaha, huku wakiwa
wanaongozwa na Roho Mtakatifu.
Itakumbukwa kwamba, kongamano la kwanza lilifanyika
kunako mwaka 1998 na kuongozwa na Mtakatifu Yohane Paulo II na Kongamano la pili likaitishwa
chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2006. Baba Mtakatifu
Francisko akizungumza na wajumbe wa kongamano hili, Jumamosi, tarehe 22 Novemba 2014
amekazia kwa namna ya pekee kabisa wongofu wa ndani na utume wa Kanisa, ni nyenzo
muhimu katika mchakato wa kumwilisha imani katika matendo.
Vyama vya kitume
na Jumuiya mpya za Kikristo zinaanza kuonesha ukomavu unaopaswa kujikita katika wongofu
ili kuendeleza dhamana ya Uinjilishaji pamoja na kuendelea kudumisha karama ya vyama
vyao vya kitume; huku wakiwapokea na kuwasindikiza wale wanaotamani kushiriki karama
hizi, ili kujenga umoja na mshikamano kwa kuzingatia uhuru wa mtu.
Baba Mtakatifu
anasema, vyama vya kitume havina budi kuendeleza karama ambayo vimepokea kutoka kwa
Roho Mtakatifu, huku vikionesha ujasiri wa kiinjili mintarafu kweli za Kiinjili na
kwamba, vinapaswa daima kurudi kwenye chemchemi ya karama zao, ili kuchota nguvu mpya
ya kukabiliana na changamoto mamboleo.
Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, vyama
hivi havina budi kuwapokea na kuwasaidia vijana wa kizazi kipya, kwa kutambua kwamba,
wao pia ni sehemu ya binadamu ambaye ana madonda makubwa moyoni mwake yanayotokana
na matizo katika familia ya binadamu, kiasi cha kukosa utambulisho na kuona ugumu
katika kufanya maamuzi magumu katika maisha. Waamini washinde kishawishi cha kuuza
uhuru wao kwa watu wengine, hali ambayo itawafanya washindwe kukua na kukomaa.
Majiundo
makini ya Kikristo yanapania kumsindikiza mwamini kwa uvumilivu na unyenyekevu mkubwa
pamoja na kusoma alama za nyakati kama anavyofanya Yesu mwenyewe. Uvumilivu ni njia
pekee kabisa ya kuonesha upendo wa kweli sanjari na kuimarisha mahusiano ya karibu
na Kristo, Yesu.
Baba Mtakatifu anasema, umoja ni paji kutoka kwa Roho Mtakatifu
na kielelezo cha neema ya hali ya juu ilitolewa na Yesu Kristo kwa njia ya Fumbo la
Msalaba, ili watu waweze kutambua kwamba, kweli ametumwa na Baba yake wa mbinguni
wakiona wafuasi wake wakiwa wameungana, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa umoja
badala ya kuendekeza kinzani na migawanyiko, kwani wote wanafanyika ndugu wamoja kutokana
na Damu Azizi ya Yesu iliyomwagika kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu.
Vyama
vya kitume na Jumuiya za Kikristo hazina budi kuwa ni sehemu ya Kanisa kwa kuheshimu
viongozi halali waliowekwa. Umoja huu ujioneshe kwa namna ya pekee katika kudumisha
misingi ya Injili ya Maisha, Familia, Amani sanjari na kusimama kidete kupinga umaskini
wa hali na kipato; kwa kukuza uhuru wa kidini na elimu ya dini. Vyama hivi vishikamane
kwa ajili ya kuganga na kuponya madonda ya utandawazi yanayomsahau Mwenyezi Mungu
na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa
vitu!
Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, ili kupyaisha karama, kuna
haja ya kuheshimu uhuru wa mtu, ili kudumisha umoja na mshikamano; mambo yanayojikita
katika wongofu wa kimissionari, nguvu inayoweza kuwasaidia kushinda mapungufu yao
ya kibinadamu, tayari kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu. Toba na wongofu wa
ndani ni njia murua kabisa ya kushiriki katika utume wa Kristo, anayewaongoza na kuwasindikiza
katika mchakato wa Uinjilishaji.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.