Umoja na mshikamano katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu!
Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu, hivi karibuni imehitimisha mkutano wake wa nane,
uliopembua kwa kina na mapana maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya
familia, yaliyofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014.
Wajumbe wameanza kudonoa kauli mbiu itakayofanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu
kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Wito na
utume wa Familia katika Kanisa na Ulimwengu mamboleo".
Wajumbe walipata bahati
ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, aliyekazia pamoja na mambo
mengine, umuhimu wa maadhimisho ya Sinodi kama kielelezo cha mshikamano wa Maaskofu
na Familia; mambo makuu yanayoendelea kufanyiwa kazi na Mama Kanisa katika maadhimisho
ya Sinodi hizi mbili.
Kardinali Lorenzo Baldisseri katika hotuba yake ya ufunguzi,
amefafanua mambo makuu yaliyojitokeza wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya
Maaskofu kuhusu familia kwamba, wajumbe wameonesha ukomavu, ukweli na mshikamano wa
kidugu, kiasi kwamba, Mababa wa Sinodi waliweza kutoa mchango wao. Hati ya Mababa
wa Sinodi inaonesha mawazo makuu yaliyojitokeza katika maadhimisho ya Sinodi hii ya
Maaskofu.
Wajumbe wanasema, wakati huu, Familia ya Mungu inapojipanga kuadhimisha
Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, kuna haja ya kuendeleza majadiliano
katika ngazi mbali mbali kuhusiana na tema zilizotolewa wakati wa maadhimisho ya Sinodi,
bila kusahau changamoto na magumu yaliyopo. Wadau mbali mbali wanaojihusisha na masuala
ya familia, washirikishwe kikamilifu, bila kusahau mchango wa vyombo vya mawasiliano
ya jamii.
Wajumbe wa Sekretarieti wametumia muda mrefu zaidi kwa ajili ya kuandaa
"Mwongozo wa Kazi" "Lineamenta" kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa
ajili ya familia. Hati hii itatumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, ili kufanyiwa
tafakari ya kina, mwanzoni mwa Mwezi Desemba 2014, ili majibu yake yaweze kurejeshwa
na kuanza kuandaa "Hati ya kutendea Kazi" yaani "Instrumentum Laboris" kabla ya kipindi
cha kiangazi cha Mwaka 2015.