Msilete makwazo kwa wale wanaotafuta huduma Kanisani!
Katika Siku kuu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni, sanjari na Maadhimisho ya Siku
ya Watawa wa Ndani, Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa
cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican amewataka wale wote wanaotekeleza utume
wao ndani ya Kanisa kuwa makini, ili kamwe wasiwe ni kikwazo kwa watu wanaotafuta
huduma, kwa kutambua kwamba, Kanisa au Hekalu ni nyumba ya Sala na Ibada, mahali ambapo
Mafumbo matakatifu yanaadhimishwa.
Waamini wengi ni watu wema, lakini wakati
mwingine wanakumbana na viongozi ambao wana uchu wa mali na madaraka na matokeo yake
wanakuwa ni vikwazo vya maendeleo ya kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anawataka Wakleri
kutekeleza wajibu wao kikamilifu na kamwe Kanisa lisigeuzwe kuwa ni soko la biashara,
hali ambayo itawafanya Wakleri kumezwa na malimwengu. Sakramenti za Kanisa ni kwa
ajili ya ustawi na maendeleo ya waamini na wala si biashara! Hakuna fedha inayoweza
kulipa thamani ya Sakramenti za Kanisa.
Baba Mtakatifu anaonya kwamba, hata
kuna baadhi ya wafanyakazi wanaotoa huduma zao ndani ya Kanisa wanaodiriki kuomba
rushwa ili kupatiwa huduma, jambo ambalo kimsingi ni kikwazo kwa waamini. Watu wamechoka
kusikia na kuona makwazo yakitendwa na viongozi wa Kanisa kutokana na uchu wa fedha.
Waamini hawawezi kuwasamehe Wakleri wanaojishikamanisha sana na fedha au wale wanaowanyanyasa
waamini wao. Hakuna mtu anayeweza kuwahudumia Mabwana wawili: Kanisa na Fedha!
Baba
Mtakatifu anasema, Yesu amekuja kumkirimia mwanadamu ukombozi kwa njia ya mateso,
kifo na ufufuko wake na wala kwa fedha, ili kuwaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu.
Kanisa linapokumbatia fedha, hapo linakwenda kinyume kabisa na utashi wa Yesu mwenyewe,
ndiyo maana Yesu alitembeza mkng'oto Hekaluni, ili kuwafukuza wale waliokuwa wamegeuza
Hekalu kuwa ni pango la wevi na wanyang'anyi. Siku kuu ya Kutolewa kwa Bikira Maria
Hekaluni, ni mwaliko kwa wote wanaohusika kuhakikisha kwamba, wanaendelea kulitakatifuza
Kanisa, ili kuwaonjesha huruma na upendo, wale wote wanaokuja kutafuta huduma kana
kwamba ni Bikira Maria.