2014-11-21 11:21:21

Mafundisho Jamii ya Kanisa ni chombo cha kukuza usawa na mshikamano!


Rais Giorgio Napolitano wa Italia amewapongeza wajumbe wanaoshiriki katika Kongamano la nne la Mafundisho Jamii ya Kanisa, Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia, kama sehemu ya mchakato unaopania kuleta mabadiliko katika maisha ya kijamii nchini Italia, hasa kwa kukabiliana na tatizo la ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wengi.

Mafundisho Jamii ya Kanisa anasema Rais Napolitano katika ujumbe wake kwamba, ni nyenzo muhimu sana inayobeba usawa na mshikamano wa kijamii, mambo ambayo yamebainishwa kwa kina na mapana katika Katiba ya Italia na Jumuiya ya Ulaya. Ni kanuni zinazopania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, mchakato wa maendeleo unajikita katika utu wa mwanadamu, ili kukabiliana na changamoto za maendeleo ya sayansi na utandawazi nchini Italia na Ulaya katika ujumla wake.

Rais Napolitano anawataka wajumbe hao kusikiliza kwa makini ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, ili waweze kushiriki kikamilifu katika ufumbuzi wa changamoto za kiuchumi nchini Italia na Ulaya katika ujumla wake. Tamasha hili limezinduliwa tarehe 20 na linatarajiwa kufungwa rasmi hapo tarehe 23 Novemba 2014. Baba Mtakatifu Francisko pia ametuma ujumbe kwa washiriki wa Tamasha hili kwa njia ya ujumbe wa video.







All the contents on this site are copyrighted ©.