2014-11-19 07:43:45

Wahamiaji wanapaswa kupokelewa na kushirikishwa katika maisha ya jamii husika!


Mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, uliofunguliwa hapo tarehe 17 Novemba 2014, unaendelea kujadili changamoto zinazowakabili wahamiaji na wageni, ili kuweza kupokelewa na kuhusishwa katika maisha ya jamii hisani. Kanisa linaendelea kuwahamasisha waamini na watu wenye mapenzi mema kushiriki katika mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji, ili kuwaonjesha upendo na huruma unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa.

Ni changamoto ya kupambana na biashara haramu ya binadamu ambayo wakati mwingine imekuwa ni chanzo kikuu cha watu kutaka kukimbilia katika nchi tajiri zaidi duniani kwa matumaini ya kupata maisha bora zaidi, lakini matokeo yake wanatumbukizwa katika mikono ya mafisadi na watu wasiokuwa na huruma wala utu! Kwa upande wa Umoja wa Mataifa, unapenda kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanapokelewa kwa kuzingia itifaki na mikataba ya kimataifa, mwaliko kwa nchi za Jumuiya ya Ulaya ili kushirikiana kwa dhati, kuokoa maisha ya wahamiaji na wakimbizi wanaokufa maji kila siku huko Baharini.

Wajumbe katika mkutano huu, wanapembua pia mwenendo unaooneshwa na wananchi kutoka katika nchi hisani kuhusiana na masuala ya wageni na wahamiaji. Wajumbe wamekumbushwa kwamba, mara nyingi wahamiaji ni watu wanaobeba machungu makubwa katika maisha yao, wakiwa na matumaini ya kupata maisha bora zaidi, kiuchumi na kijamii, ili siku moja, hata wao waweze kuhesabika miongoni mwa watu waliobahatika kuonja raha baada ya taabu na mahangaiko yao ya ndani. Ikiwa kama wahamiaji hawa watapokelewa na kuonjeshwa ukarimu, wanaweza kutoa mchango mkubwa kwa nchi wahisani na kule wanakotoka.

Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, Ufilippini ambaye pia ni mjumbe wa Baraza hili ya Kipapa anasema, nchi yake ni kati ya nchi ambazo zinazalisha wahamiaji wengi duniani, kumbe uhamiaji ni dhana inayopaswa kuchambuliwa katika mapana yake mintarafu mtazamo wa Kanisa Katoliki, ili kuweza kuwashirikisha wahamiaji katika maisha na utume wa Kanisa mahalia, kwa kuheshimu na kuthamini taratibu na kanuni za Makanisa mahalia. Wahamiaji wanaotafuta maisha bora katika uchumi ni mada ambayo imevuta hisia za wajumbe wengi, kutokana na shuhuda zilizotolewa na baadhi ya wahamiaji kutoka Brazil, Taiwan na Italia.







All the contents on this site are copyrighted ©.