2014-11-19 07:22:38

Mshikamano na wagonjwa wenye mtindio wa ubongo!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 22 Novemba 2014 atakutana na kuzungumza na wagonjwa pamoja na wadau mbali mbali wanaotekeleza utume wao miongoni mwa watu wenye mtindio wa ubongo. Ataonja na kusikiliza shuhuda zinazotolewa na wagonjwa wa mtindio wa ubongo pamoja na familia zao, huku wakisaidiwa na vyama vya kitume, ili kupata tiba na haki zao msingi kwa kushirikiana na wataalam katika sekta ya afya kimataifa.

Tukio hili litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI mjini Vatican litakuwa ni kilele cha maadhimisho ya mkutano mkuu wa ishirini na tisa, unaofanywa na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Wagonjwa wenye mtindio wa ubongo: kuhamasisha matumaini". Mkutano huu unaowashirikisha mabingwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia unafunguliwa rasmi Alhamisi tarehe 20 Novemba 2014.

Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican siku ya Jumanne, tarehe 18 Novemba 2014. Mkutano huu ni kielelezo makini kwamba, Kanisa litaendelea kushikamana na watu wanaoteseka kutokana na magonjwa mbali mbali.

Ugonjwa wa mtindio wa ubongo unagumishwa na ujinga pamoja na unyanyapaa, ndiyo maana Kanisa linapenda kushughulikia ugonjwa huu kwa kuwashirikisha watafiti, watalaam na mabingwa, ili kuweza kuuchambua ugonjwa huu kitabibu, kisaikolojia, kifamilia na kijamii, na hatimaye kubainisha mikakati ya kichungaji na maisha ya kiroho. Mama Kanisa anapenda kuwahimiza wanasayansi, familia, shule na vyama vya kitume, kushikamana na wagonjwa wenye mtindio wa ubongo.

Kilele cha mkutano huu, itakuwa ni siku ya sala, tafakari pamoja na kusikiliza shuhuda mbali mbali zitakazokuwa zinatolewa na wadau mbali mbali ambao wanaoishi na wagonjwa wenye mtindio wa ubongo, kama kielelezo makini cha upendo na mshikamano. Kutakuwa na maonesho ya kazi zilizofanywa na watu mbali mbali. Siku tatu muhimu za kazi, zitaweza kuwaunganisha watu mbali mbali katika majadiliano, huku wakibadilishana mawazo, kwa lengo la kutaka kukaa karibu na wagonjwa wa mtindio wa ubongo, ili kuwajengea matumaini, kama anavyosema Padre Augusto Chendi, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya.

Monsinyo Jean Marie Mate Musivi Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza hili anasema, mkutano huu wa kimataifa ni fursa makini ya kuweza kutafakari na kushirikishana: ujuzi, uzoefu na mang'amuzi, ili kuimarisha sera na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa wenye mtindio wa ubongo. Lengo ni kuwawezesha wadau mbali mbali kutambua kwamba, kiini cha mambo yote haya ni binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, mwenye utu na heshima yake, licha ya magonjwa yanayomwandama.







All the contents on this site are copyrighted ©.