2014-11-19 09:30:20

Mabadiliko na changamoto katika sekta ya kilimo vijijini!


Kardinal Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, hivi karibuni, alishiriki katika ufunguzi wa kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Shirikisho la Waamini wa Kanisa Katoliki katika maisha ya Wakulima Vijijini, lililoanzishwa kunako mwaka 1923. Hili ni Shirikisho linalowaunganisha Maaskofu, Watawa na Waamini Walei wanaotekeleza mikakati yao kichungaji kati ya wakulima wanaoishi vijijini nchini Marekani. RealAudioMP3

Katika kongamano hili, wajumbe wamepata fursa ya kujadili kwa kina mapana mabadiliko yanayoendelea kutokea katika sekta ya kilimo mintarafu changamoto zinazoibuliwa na utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia katika viwanda pamoja na teknolojia ya viumbe hai. Mambo yote haya yanatoa changamoto kubwa kwa wadau mbali mbali katika sekta ya kilimo, hasa katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, kuna uhakika wa usalama wa chakula pamoja na lishe bora kwa idadi ya watu inayoendelea kuongezeka maradufu kadiri ya takwimu za Umoja wa Mataifa.

Kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira, bado Kanisa lina mchango mkubwa katika kuwafunda waamini na watu wote wenye mapenzi mema utunzaji bora wa mazingira, kama ushiriki wa mwanadamu katika kuendeleza kazi ya uumbaji ambayo amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao yake kwa kizazi kijacho. Mabingwa wa kilimo, mazingira na wakulima wenyewe, wameshirikisha uzoefu na mang’amuzi juu ya mambo ambayo yanayopaswa kutekelezwa ili kukabiliana na changamoto za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kongamano hili ni sehemu ya utangulizi kwa ajili ya maadhimisho ya kongamano la kimataifa kuhusu chakula, litakalofanyika Milano, Italia kunako mwaka 2015, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kulisha Dunia”.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba ya Kardinali Peter Turkson na Dr. Michael Czerny, amekazia mchango mkubwa uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Nyaraka zake msingi, zinazoonesha kwamba, Kanisa kwa kutumia Mapokeo na rasilimali yake litaendelea kumsindikiza mwanadamu katika mapitio mbali mbali ya maisha; wakati wa furaha, shida na mahangaiko, ili kuwajengea tena imani na matumaini.

Kanisa litaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali katika maboresho ya uhakika na usalama wa chakula duniani, kwa kuonesha mshikamano wa pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii hasa kutokana na baa la njaa na umaskini wa hali na kipato. Kuundwa kwa Baraza la Kipapa la haki na amani ni kuliwezesha Kanisa kuendeleza mchakato wa maendeleo endelevu yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa kuzingatia kanuni za haki jamii kimataifa pamoja na ushuhuda wa mshikamano na upendo unaotolewa na Mama Kanisa.

Kardinali Turkson anasema, Kanisa linapenda kukuza na kudumisha majadiliano na wadau mbali mbali, lakini zaidi na wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kutambua umuhimu wa kudumisha kanuni maadili katika sekta ya kilimo na uzalishaji viwandani pamoja na utunzaji bora wa mazingira; kwa lengo la kutaka kumhudumia binadamu katika mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili. Majadiliano kati ya watu ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao pamoja na kutafuta mafao ya wengi.

Viongozi wanapaswa kutambua kanuni msingi zitakazowawezesha kutafuta mafao ya wengi ndani ya jamii, kwa kushirikiana na wadau mbali mbali katika masuala ya chakula, mazingira na imani. Kanisa linatambua kwamba, chakula ni jambo la muhimu kwa kila binadamu kwani linajikita katika kanuni maadili, maisha ya kijamii na kibinadamu, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kulinda na kudumisha sekta ya kilimo katika uzalishaji, ugavi na matumizi ya chakula.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alionya kwamba, kuna watu wachache wanaomiliki maeneo makubwa ya ardhi; wanaotumia vyanzo vya maji kwa mafao ya binafsi pamoja na pembejeo, hali ambayo imeendelea kusababisha kashfa ya baa la njaa duniani, wakati kuna watu wanakula na kusaza kiasi hata cha kufanya kufuru. Mama Kanisa anapenda kujadiliana na wadau mbali mbali kwa kuangalia kwa kina na mapana kanuni maadili zitakazosaidia kutokomeza baa la njaa duniani, kuwa na uhakika wa uzalishaji na usambazji wa chakula na lishe bora.

Je, ni mbinu gani zinaweza kutumika ili kulinda utu na heshima ya wakulima sehemu mbali mbali za dunia? Je, ni kwa jinsi gani, vyanzo vya maji, ardhi n arasilimali mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu zinaweza kutumika kwa ajili ya mafao ya wengi? Je, ardhi inaweza kuwa ni kwa mafao ya wengi ili kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani?

Kardinali Peter Turkson anasema, maswali haya ni muhimu sana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inakuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa siku za usoni, sanjari na utunzaji bora wa mazingira, changamoto inayomwandama mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.