Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, 19 Novemba 2014 kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameendelea kutafakari kuhusu
Kanisa, lakini kwa kukazia wito wa utakatifu unaotolewa kwa waamini wote, kutokana
na dhamana ya Ubatizo, kila mwamini anatakiwa kuwa Mtakatifu.
Baba Mtakatifu
anakumbusha kwamba, utakatifu kwanza kabisa ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na
wala si matunda ya juhudi za mtu binafsi. Mtakatifu Paulo anakumbusha kwamba, Yesu
alilipenda Kanisa kiasi cha kujisadaka, ili liweze kuwa takatifu. Kwa njia ya umoja
na Kanisa, kila Mkristo ametakatifuzwa kwa neema ya Sakramenti ya Ubatizo na hivyo
anatakiwa kukua na kukomaa katika utakatifu.
Waamini wanaalikwa kumwilisha
hafuru ya utakatifu katika medani mbali mbali za maisha yao ya kila siku, wanapotekeleza
dhamana na majukumu, daima wajiweke katika hali ya sala, huku wakiwa wameungana na
Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao. Baba Mtakatifu anawauliza waamini na wote wenye
mapenzi mema ni kwa kiasi gani wamejizatiti katika kuchuchumilia wito wa utakatifu
wa maisha? Ili kuishi katika utakatifu, Yesu anawaalika wafuasi wake kuonja furaha
inayobubujika kutoka kwake, ili waweze kuwaonjesha wengine mapendo.
Mtu anapokua
na kukomaa katika utakatifu, ina maana kwamba, anakuwa ni mtu mwema zaidi, asiyezongwazongwa
na ubinafsi na hali ya kujitafuta mwenyewe na daima yuko tayari kujisadaka kwa ajili
ya huduma kwa wengine kama wakili mwema wa neema mbali mbali za Mungu. Amewataka waamini
kujenga na kuimarisha upendo na mshikamano kati yao, kwa kutambua kwamba, Yesu daima
anaendelea kuambatana nao katika hija ya maisha yao ya kiroho, ili siku moja waweze
kuwa watakatifu, huku wakiendelea kuonesha uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake.
Baba
Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa wajumbe wanaoshiriki katika Jukwaa la Uchumi
Duniani, linaloendeshwa na Vyuo vikuu vya Kipapa mjini Roma, ili kuisaidia Jamii kuondoka
na mambo ambayo yanawatenga wengine katika mchakato wa kiuchumi, kwa kutumia nguvu
ya fedha, ambayo kwa baadhi ya watu imekuwa kama miungu wadogo. Fedha anasema Baba
Mtakatifu inapaswa kutumika kwa ajili ya mafao ya wengi.