Fanyeni maamuzi magumu ili kujenga upatanisho na amani!
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 19 Novemba 2014
ameonesha masikitiko yake kutokana na kinzani za kidini na kijamii zinazoendelea kujitokeza
katika Nchi Takatifu, kwa matukio ya mauaji ambayo yamepelekea walimu wanne wa dini
ya Kiyahudi kupoteza maisha.
Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wale wote
walioguswa na matukio haya ya kinyama uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Kutoka
katika undani wa moyo wake, anapenda kuwaalika wote wanaohusika kuachana na vitendo
hivi vinavyosababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, kwa kufanya maamuzi magumu
yanayojikita katika upatanisho na amani. Kujenga misingi ya amani ni kazi kubwa, lakini
kuishi kwa amani, kweli yataka moyo!
Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba hapo tarehe 21 Novemba, Kanisa litaadhimisha
Siku kuu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni, sanjari na Siku ya Watawa wa Ndani, inayojulikana
kwa lugha ya Kilatini, "Pro Orantibus".
Baba Mtakatifu anasema, hii ni fursa
makini kwa Mama Kanisa kuwakumbuka na kuwaombea watawa wanaoendelea kujisadaka kwa
ajili ya Mungu na jirani, katika sala na ukimya mtakatifu, huku wakitambua na kuthamini
ukuu wa Mungu anayepaswa kupendwa na kuheshimiwa na wote. Ni wakati wa kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa shuhuda zinazotolewa kwa njia ya maisha ya Watawa wa ndani, mwaliko
wa kuhakikisha kwamba, wanapata mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili, ili waendelee
kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa Kristo na Kanisa lake.