2014-11-18 11:40:07

Tanzania inakabiliana na changamoto nyingi, salini, ili yote yaende salama!


Dr. James Msekela, Balozi wa Tanzania nchini Italia anawaalika viongozi wa kidini na waamini mbali mbali kushikamana kwa pamoja ili kuiombea Tanzania wakati huu inapokabiliana na changamoto mbali mbali, ambazo kwa hakika zinahitaji kusimamiwa na kuongozwa kwa mkono wa Mwenyezi Mungu, ili Tanzania iendelee kuwa kweli ni kisiwa cha amani! RealAudioMP3

Dr. Msekeleza ameyasema hayo, Jumapili tarehe 16 Novemba 2014 alipokutana na kuzungumza na Jumuiya ya Wanafunzi Wakatoliki wanaosoma mjini Roma, mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kikanisa cha Seminari kuu ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia.

Nabii Isaya katika Sura ya kwanza, Mstari wa nne anasema kwa msisitizo kwamba "Ole wake Taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu! Wamemwacha Bwana, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma... Kama Bwana wa majeshi asingelituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora."

Dr. Msekela anaamini kwamba, mabaki machache yanayozungumzwa kwenye sehemu hii ya Neno la Mungu ni viongozi wa kidini, ambao wanadhama ya kuhakikisha kwamba, wanaliombea Taifa ili liweze kukabiliana na changamoto za uchaguzi wa Serikali za mitaa unaofanyika mwaka 2014; Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika kunako mwaka 2015; Kura ya maoni kuhusiana na Muswada wa Katiba Mpya ya Tanzania ambayo imepitia kipindi kigumu cha malumbano na kejeli za kisiasa.

Viongozi wa kidini mara nyingi wameonesha nia njema, mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Viongozi wa kidini na waamini wote katika ujumla wao, waungane, ili taifa la Tanzania liweze kukabiliana na changamoto hizi kwa ukomavu, ili kweli yote yaende kadiri ya mpango wa Mungu kwa watanzania.







All the contents on this site are copyrighted ©.