2014-11-18 07:37:16

Simameni kidete kupinga biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 16 Novemba 2014 amekutana na kuzungumza na vijana waliokuwa wanashiriki katika kongamano la kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu lililokuwa limeandaliwa na Taasisi ya kipapa ya Sayansi kwa kuwashirikisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu amewataka vijana kusimama kidete bila kuyumba, ili kupambana kufa na kupona dhidi ya biashara haramu ya binadamu inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kumgeuza binadmu kuwa kama bidhaa, inayoweza kuuzwa, kununuliwa au kutupwa katika taka!

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, mbele ya Mwenyezi Mungu, kila mtu anaheshimiwa kutokana na utu wake kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na wala hakuna takataka. Hii ni changamoto kwa vyama vya kitume vinavyojibidisha katika mchakato wa kupambana na biashara haramu ya binadamu kusonga mbele bila ya kuchoka.

Baba Mtakatifu amewapongeza wale wote ambao wameendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Haitoshi kwa vijana kushiriki katika mapambano haya, bali kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza ili kweli utu na heshima ya binadamu viweze kuthaminiwa na kuheshimiwa na wengi. Maisha yanapata maana ya pekee ikiwa kama yatamimimwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengine.

Vijana hao baada ya kuhitimisha Kongamano hili la siku mbili lililofunguliwa hapo tarehe 15 hadi tarehe 16 Novemba 2014, wametoa tamko la pamoja linalolaani biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo yanayoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Wanapenda kuonesha mshikamano wao wa dhati na waathirika wa vitendo hivi vya kinyama, kwa kuwataka vijana kufungua macho na masikio yao, ili kulaani tamaduni na wale wote wanaojihusisha na vitendo hivi vya kinyama.

Wanawapongeza vijana wanaofanya kazi zao kwa heshima na taadhima na kwamba, kongamano hili la kimataifa limekuwa kama mwanga katika hija ya maisha yao, ili kuwakirimia matumaini tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia wale wanaoteseka kutokana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Hawa ni watu wanaopaswa kusikilizwa, kusaidiwa na kuhudumiwa, ili wasiendelee kutumbukizwa katika utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu.

Vijana wanazitaka serikali zao kuwajibika barabara katika ulinzi na usalama wa raia zao, kwa kuwapatia mafunzo ya dhati wafanyakazi Serikalini na watumishi katika vyombo vya ulinzi na usalama, ili kuweza kukabiliana na tatizo la biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Serikali zisimame kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; ziwasaidie waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, sanjari na kutenga rasilimali watu na fedha ili kupambana na janga hili ambalo ni kero kubwa kwa utu na heshima ya binadamu.

Vijana wanasema, kuna haja kwa serikali mbali mbali kuunda kikosi kazi kitakachokuwa na dhamana ya kudhibiti biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; nyanyaso na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana pamoja na kuwaelimisha watu kwa kutumia vyombo vya mawasiliano ya jamii, umuhimu wa kulinda na kuheshimu utu wa mwanadamu. Njia za mawasiliano zisaidie kuleta mabadiliko ya kweli katika tamaduni na maisha ya watu kwa kukataa katu katu kushiriki katika mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Ili kufikia lengo hili, vijana katika tamko lao wamewataka kuwepo na kampeni itakayosaidia kuwafunda waalimu, ili waweze kutoa elimu makini, itakayowasaidia vijana kuheshimiana na kuthaminiana na kwamba, tendo la ndoa ni takatifu na wala si biashara. Jamii inapaswa kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia wanazokumbana nazo wanawake na wasichana katika jamii zao.

Jamii nzima inawajibika kushikamana ili kuondoa kero na nyanyaso hizi dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Vijana wanavitaka vyombo vya dola kuwashughulikia wafanyabiashara na wateja wa ngono, ili kuvunjilia mbali mnyororo wa kashfa na mateso yanayosabishwa na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.