Bwana Michael Kafando ameteuliwa kuwa ni Rais wa Burkina Faso katika kipindi cha mpito
kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo Mwezi Novemba 2015. Bwana
Kafando ni mwanadiplomasia mkongwe aliyewahi kuwa Waziri wa mambo ya nchi za nje na
Mwakilishi wa kudumu wa Burkina Faso kwenye Umoja wa Mataifa.
Muafaka huu
kati ya Jeshi, Wanasiasa na Viongozi wa kidini umefikiwa rasmi hapo tarehe 16 Novemba
2014 baada ya wadau mbali mbali kuweka sahihi ya makubaliano yaliyotoa mwanya kwa
Bwana Michael Kafando kuteuliwa ili kuongoza nchi, baada ya kuwapepeta viongozi wengine
waliokuwa wamependekezwa katika kinyang'anyiro cha urais nchini Burkina Faso.
Kazi
kubwa inayomngoja Rais Kafando kwa sasa ni kuteuwa mtu atakayekuwa Waziri mkuu wa
kipindi cha mpito atakayepewa dhamana ya kuteuwa Mawaziri ishirini na watano watakaounda
Serikali ya mpito. Bunge jipya litaundwa na wabunge tisini watakaochaguliwa kutoka
katika makundi mbali mbali nchini Burkina Faso.