Wahamiaji ni rasilimali na wala si kero wala majanga tu!
Kongamano la Saba la Kimataifa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji linaloongozwa
na kauli mbiu “ushirikiano na maendeleo katika shughuli za kichungaji miongoni mwa
wahamiaji”, linalowashirikisha mabingwa na wataalam 300 kutoka katika nchi 93, kuanzia
tarehe 17 hadi tarehe 21 Novemba 2014 linafanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha
Urbaniana, kilichoko mjini Roma.
Kilele cha kongamano hili ni hapo tarehe
21 Novemba, 2014 wajumbe watakapopata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu
Francisko mjini Vatican.
Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la
Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi
maalum katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha kwamba, uhamiaji ni tatizo nyeti,
kwani wahamiaji ni watu ambao wamebeba ndani mwao: karama, matumaini na matatizo na
changamoto za maisha.
Ikiwa kama wahamiaji watatambuliwa na kuthaminiwa wanaweza
kuwa ni kichocheo kikuu cha ugunduzi na maendeleo endelevu kati ya watu na kamwe wasichukuliwe
kuwa ni kero na mzigo katika jamii wahisani. Hawa ni nguvu kazi ambayo ikitumiwa barabara
inaweza kusaidia katika mchakato wa uzalishaji, ni chem chemi ya ushirikiano na umoja
kati ya tamaduni, Kanisa na Serikali husika.
Ni watu wanaopaswa kufunda barabara,
kupewa fursa za ajira na kushirikishwa kikamilifu katika jamii inayowahifadhi, hapo
watakuwa ni watu wenye mafao kwa jamii hisani na kule walikotoka.
Kardinali
Veglio’ anakiri kwamba, kati ya changamoto kubwa inayoikabili Jumuiya ya Kimataifa
ni kusimamia na kuratibu shughuli za wahamiaji na wakimbizi. Wahamiaji wanakabiliana
na changamoto mbali mbali katika medani za kiuchumi, kijamii, kitamaduni na kidini.
Wahamiaji wasipodhibitiwa vyema, wanaweza kuwa ni chanzo kikuu cha uhalifu na uvunjaji
wa sheria na kanuni za maisha ya watu, hali ambayo wakati mwingine imekuwa ni chanzo
cha woga usiokuwa na mashiko wala ustaarabu.
Wahamiaji wamekuwa ni chanzo kikuu
cha ukuzaji wa uchumi kwa nchi hisani na kule wanakotoka kwani wanapopata ajira, sehemu
ya mapato yao, inarudishwa nchini mwao kwa ajili ya kusaidia maboresho ya maisha ya
familia na jamii kwa ujumla. Ni kundi kubwa linalochangia pia ustawi na maendeleo
ya Kanisa zima.
Kardinali Veglio’ anasema kwamba, “familia ya wahamiaji” ni
kati ya mada nyeti zinazojadiliwa katika kongamano la saba la wahamiaji kimataifa.
Hii inatokana na ukweli kwamba, Mama Kanisa anaendelea kuwekeza zaidi katika familia,
ili kuiwezesha familia kutangaza Injili ya Familia na matumaini kwa wale waliokata
tamaa. Itakumbukwa kwamba, familia ni chemchemi ya maisha, tamaduni, tunu msingi za
maisha ya kiutu na kiimani. Ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, Kanisa linasaidia kuganga
na kuponya madonda ya familia za wahamiaji, ili ziweze kutekeleza dhamana na utume
wake katika jamii husika, kwa kushirikiana na nchi wanakotoka wahamiaji hawa.
Katika
mkutano huu, wajumbe pia wanajadili kwa kina na mapana kuhusu dhamana na wajibu wa
wanawake katika suala zima la uhamiaji kwa kutambua kwamba, wahamiaji wanawake wanaunda
takribani asilimia 49% ya wahamiaji wote duniani. Ni kundi linalotafuta ustawi na
maendeleo ya watu wake. Wanawake wakithaminiwa wanaweza kuwa ni vichocheo vya ushirikiano
na maendeleo ndani ya jamii.
Kanisa linatambua matatizo na changamoto wanazokabiliana
nazo wanawake wanaolazimika kuzihama nchi zao kwa kuacha familia na wakati mwingine
wanajikuta wakitumbukizwa kwenye biashara haram ya binadamu na utumwa mamboleo. Vijaana
wanaohama kutoka katika nchi zao wakitafuta maisha bora zaidi wanaendelea kuongezeka
maradufu, huku wakiwa wamebeba ndani mwao karama na vipaji mbali mbali tayari kushiriki
katika mchakato wa maboresho ya kijamii.
Vijana wanapaswa kulindwa na kutunzwa,
ili waweze kushirikisha ndoto na mang’amuzi yao ya maisha, kwa ajili ya ustawi na
mafao ya wengi. Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele kuwalinda na kuwatetea vijana
wahamiaji katika shida na mahangaiko yao, ili waweze kuwa imara katika utambulisho
na imani yao.
Kardinali Veglio’ anasema kwamba, changamoto kubwa kwa sasa ni
kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya wahamiaji na wakimbizi inalindwa na kutetewa
na wengi. Kanisa linapania pamoja na mambo mengine, kuwajengea uwezo waamini ili waweze
kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wakimbizi na wahamiaji. Wawasaidie wakimbizi
na wahamiaji katika maboresho ya maisha mapya wanapokuwa ugenini, hasa zaidi wanapokumbana
na matatizo pamoja na changamoto za maisha.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.