2014-11-17 09:12:00

Ujio wa Papa Francisko nchini Ufilippini ni baraka na neema!


Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ufilippini ni baraka na neema kwa wananchi wa Ufilippini, hususan maskini, wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na wale wpte walioguswa na majanga asilia na yale ambayo yanaendelea kusababishwa na binadamu, bila kusahau ukosefu wa haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume, ataweza kuwaonjesha wananchi wa Ufilippini, ile sura ya Yesu Kristo mchungaji mwema, aliyejisadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili kumshirikisha maisha ya uzima wa milele.

Hija hii anasema Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila kwamba, ni baraka, lakini inayobeba pia wajibu na dhamana kubwa. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Sri Lanka kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 15 Januari 2015 na baadaye kutembelea nchini Ufilippini hadi tarehe 19 Januari 2015. Ni hija itakayowachangamotisha waamini kuwa karibu zaidi na Yesu Kristo kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu ndani ya jamii.

Kardinali Tagle anasema, wafuasi wa Yesu wakiwa wanasukumwa na nguvu ya Roho Mtakatifu, watahamasishwa zaidi kutoka kifua mbele, ili kuwaendea wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na umaskini, ujinga na maradhi. Watakuwa na wajibu wa kuwaganga watoto wenye madonda makubwa katika maisha yao, familia zenye shida, kinzani na migogoro; kwa kuwaheshimu na kuwathamini hata wale wanaotofautiana nao kwa mawazo, maneno na matendo.

Waamini watakuwa na wajibu wa kuwafunda vijana, ili waweze kutumia uhuru wao kwa kuwajibika barabara, huku wakipembua kwa kina na mapana mchango wao katika kulinda na kutunza mazingira; kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kitamaduni kwa kukumbatia tunu msingi za maisha bora ya kijamii na kiutu, huku wakionesha wema na huruma, mambo yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa kushikakamana na kutembea pamoja na Baba Mtakatifu Francisko, Kanisa nchini Ufilippini linataka kueneza Injili ya Matumaini na Furaha kwa wale waliokata tamaa na kuelemewa na majonzi katika maisha.

Kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Ufilippini ni huruma na wema. Kardinali Luis Antonio Tagle anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuishi mintarafu tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu ambazo zimeimarishwa kwa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha; kwa kushiriki katika Mafumbo ya Kanisa, ili kujichotea neema na baraka katika maisha, hasa katika Ekaristi Takatifu, chimbuko na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni changamoto ya kujipatanisha na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani, kwa kujikita katika matendo ya haki na upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.